Na Mathias Canal, Kiteto-Manyara
Mbunge wa Jimbo la Kiteto Mkoani Manyara Mhe Edward Ole Lekaita amempongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa Bilioni 1.104 kwa ajili ya ujenzi wa shule Shikizi katika Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara.
Mhe Ole Lekaita ametoa pongezi hizo kwa Rais Samia leo tarehe 23 Septemba 2023 wakati akizungunza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Ngaikitala kata ya Sunya akiwa katika ziara ya siku tatu kwenye jimbo la Kiteto.
Amesema kuwa hiyo ni ishara ya upendo mkubwa wa Rais Samia kwa wananchi wa Kiteto na Tanzania kwa ujumla kwani mambo ya maendeleo anayoyafanya wilayani Kiteto yanafanyika katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema kuwa katika kata hiyo ya Sunya serikali ilitoa Milioni 108 kwa ajili ya ujenzi wa Shule shikizi Ngaikitali, Milioni 138 kwa ajili ya shule shikizi Mbalibali na Milioni 88 kwa ajili ya ujenzi wa shule shikizi ya Lengale.
Amesema kuwa katika jamii ya wafugaji hususani Wamasai sio jambo jepesi kusoma, lakini amewaomba wananchi kuhakikisha wanawapeleka watoto shule huku akipiga marufuku utoroshaji wa watoto.
Mbunge Ole Lekaita amesema kuwa kiasi hicho cha Bilioni 1.104 kimewezesha ukamilishaji wa shule shikizi 18 jambo ambalo limetatua kadhia ya utoaji elimu katika jamii hiyo ya Wilaya ya Kiteto.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment