METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, July 4, 2023

RC SINGIDA ATAKA NGO’s ZINAZO KWENDA KINYUME NA UTAMADUNI WA KITANZANIA ZICHUKULIWE HATUA KALI ZA KINIDHAMU

Mkuu wa Mkoa wa Singida,Peter Serukamba (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO's) Mkoa wa Singida baada ya kufungua kongamano la Jukwaa la mashirika hayo mkoani hapa lililofanyika Ukumbi wa Hoteli ya KBH Julai 3, 2023.

Na Dotto Mwaibale, Singida 

MKUU wa Mkoa wa Singida,Peter Serukamba ameagiza Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali mkoani hapa kuzichukulia hatua za kinidhamu Azise ambazo zinafanya mambo ambayo hayaendani na Tamaduni za Kitanzania. 

Serukamba alitoa agizo hilo jana Julai 3, 2023 wakati akifungua kongamano la Jukwaa la mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO's) Mkoa wa Singida lililofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya KBH mjini hapa. 

Alisema Azise zipo nyingi ambazo zinafanya vizuri lakini zipo ambazo hazifanyi vizuri na kukiuka taratibu na sheria za nchi. 

" Mchukue hatua za kinidhamu  kulingana na mwongozo wa mashirika kwa baadhi ya mashirika yanayoendesha shughuli zao kinyume na sheria za nchi,". alisema Serukamba. 

Serukamba aliyakumbusha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (AZISE) kufuata misingi ya katiba, sheria na kanuni zilizowekwa katika utekelezaji wa majukumu yao na kuliomba baraza la mashirika hayo kusimamia vema uendeshaji wa mashirika hayo kuanzia ngazi za chini na kufungamanisha taarifa za utekelezaji wa AZISE na taarifa za serikali zinazowasilishwa ngazi zote ili jamii ione tija ya utekelezaji wa AZISE. 

Awali akisoma risala ya jukwaa hilo mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, Mkurugenzi wa Shirika la REDO, Hudson Kazonta alisema katika kipindi cha mwaka 2022 mashirika hayo yametoa takribani jumla ya ajira 400 na kuwa ajira hizo ni mojawapo ya njia ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kutengeneza ajira kwa wananchi wake. 

Alisema pamoja na mambo mengine, mashirika hayo (AZAKI) yamekuwa yakiwajengea uwezo wahitimu wanaomaliza vyuo mbalimbali ili kuwawezesha kupata uzoefu katika utendaji kazi ambapo jumla ya vijana takribani 150 wamenufaika na jambo hilo katika nyanja mbalimbali. 

Aidha, Kazonta alisema katika utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa mwaka 2022 jumla ya takribani Sh. Billioni 8 zimetumika kutekeleza miradi hiyo Mkoa wa Singida katika afua za Afya, Elimu, Msaada wa kisheria, Usawa wa Kijinsia, Vijana, Wanawake na watu wenye Ulemavu, Kilimo, Watoto, Mazingira, Maji na Usafi wa Mazingira, Utawala Bora, Mabadiliko ya Tabia Nchi pamoja na uwezeshaji jamii kiuchumi. 

Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) Onesmo Ole Ngurumwa alisema Asasi za kiraia ni kiungo kikubwa sana katika maendeleo ya Taifa na duniani kote kwani historia ya dunia haiwezi kuzungumzwa bila ya kuwepo asasi hizo. 

Alisema duniani kuna sekta tatu ambazo zinaunda taifa lolote lile na kuzitaja kuwa ni Serikali, Wafanyabiashara na sekta za kijamii na kuwa mara jingi sekta ya kijamii imekuwa haieleweki vizuri licha ya kuwa na mchango mkubwa katika kusukuma gurudumu la maendeleo.

Alisema changamoto kubwa iliyopo ni suala la kodi na wamekuwa wakiwasiliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuangalia kuwa wao kama sekta au mkono wa pili wa serikali  katika kusaidia shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii nchini waondolewe zile kodi pingamizi ukiachilia mbali za ajira kwa wafanyakazi wao ambazo ni lazima zilipwe. 

Alitaja msamaha wa kodi ambao wanaomba wasamehewe ni wakiingiza magari kutoka nje ya nchi ambayo yanakwenda kutumika vijijini kwa ajili ya shughuli za maendeleo na vitu vingine vinavyofanana na hivyo.

Mjumbe wa Baraza la Mashirika Yasiyokuwa  ya Kiserikali (NACONGO), Peter Lisu alisema lengo kubwa la kukutana ni kujengeana uwezo katika masuala ya kodi na kupeana mbinu mbalimbali za utendaji wa kazi wa mashirika hayo, kuona fursa ambazo zitatoa mchango wa kuendeleza shughuli maendeleo mkoani Singida.

Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) Onesmo Ole Ngurumwa (katikati) akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida wakati alipokuwa akitembelea mabanda kuona shughuli mbalimbali zinazofanywa na mashirika hayo.
Mkurugenzi wa Shirika la Jiokoe na Umaskini yaani Stars of Poverty Rescue Foundation, Tanzania (SPRF) lililopo mkoaniSingida Dk. Suleiman Muttani, akitoa maelezo kwa mkuu wa mkoa (Aliyekaa)baada ya kutembelea banda la shirika hilo.

Fundi wa majiko Sanifu, Musa Nasoro (kulia) akitoa maelezo kwa mkuu wa mkoa alipotembelea banda la fundi huyo.
Wajasiriamali waliowezeshwa na mashirika hayowakionesha bidhaa zao
Mjasiriamali Pendo Samuel aliyenufaika na mashirika hayo akionesha bidhaa zake kwa mkuu wa mkoa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika  lisilokuwa la Kiserikali la Save the Mother and Children of Central Tanzania (SMCCT), Evalyen Lyimo (katikati) akimueleza mkuu wa mkoa kazi zinazofanywa na shirika hilo.
Washiriki wakiwa kwenye kongamano hilo.
Kongamano likiendelea.
Mjumbe wa Baraza la Mashirika Yasiyokuwa  ya Kiserikali (NACONGO), Peter Lisu, akizungumza kwenye kongamano hilo.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Singida, Patrick Kasango akiongoza kongamano hilo.
Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) Onesmo Ole Ngurumwa, akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo.
Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Singida sehemu ya  Rasilimali Watu, Stephen Pankras akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa mkoa huo, Dk.Fatuma Mganga.
Mkurugenzi wa Shirika la REDO, Hudson Kazonta, akisoma risala ya mashirika hayo kwa mgeni rasmi.
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mragili akizungumza wakati akimkaribisha mkuu wa mkoa kutoa hutuba yake ya ufunguzi.
Taswira ya kongamano hilo.
Picha ya pamoja na mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba (katikati) waliokaa.
 

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com