METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, June 5, 2023

Wabunge waipongeza Wizara, wataka itumie michezo kutangaza utalii, waishauri Serikali kurejesha visiwa na fukwe wizara ya Maliasili


Na John Mapepele

Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mapinduzi  makubwa yanayofanywa  hivi sasa  chini ya Uongozi wa Waziri Mohamed Mchengerwa na kuitaka  wizara hiyo iongezewe  bajeti ili iweze kufanya  vizuri zaidi katika mwaka wa fedha 2023/24, huku wakipongeza kazi  nzuri  iliyofanywa  na Rais Samia Suluhu Hassan ya kutangaza  utalii  kimataifa.

Pongezi hizo zimetolewa leo Mei 5, 2023 na wabunge takribani wote wakati  wanachangia   katika siku ya pili kwenye  Hotuba  ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Bajeti  ya Wizara ya Maliasili  na Utalii  ya mwaka 2023/24 iliyowasilishwa  bungeni na Mhe. Mohamed Mchengerwa Mei 2, 2023.

Akichangia katika hotuba hiyo, Mbunge wa viti maalum Njombe (CCM) Neema Mgaya ameitaka Serikali kuangalia namna ya  kurudisha  fukwe na visiwa vyote katika Wizara  ya Maliasili na Utalii ili visimamiwe na Bodi ya Utalii nchini  ili kuweza  kuuza utalii wa nchi kwa pamoja kama inavyofanyika katika nchi nyingi duniani.

Aidha, amesema nchi kama Ushelisheli zimekuwa zikitegemea utalii wa fukwe  na bahari  pekee ambapo amefafanua  kuwa Tanzania  imebarikiwa kuwa  na  fukwe nzuri kuliko nchi nyingi duniani na endapo zitasimamiwa  vizuri zitakuwa na mchango  mkubwa kwenye uchumi.


Kwa upande mwingine Mhe. Mgaya ameishauri Serikali kuona umuhimu wa  kujenga  mahoteli  kwa ajili ya  kuwalaza wageni ambao wameanza kumiminika kufuatia mikakati mizuri iliyowekwa  na Wizara  na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  kupitia Filamu ya The Royal Tour.

Naye, Mhe. Benedetha Mshashu ameipongeza Wizara na Serikali kwa ujumla kwa  mikakati ya kukuza  na kutangaza utalii na amesema  imezaa matunda ambapo ameomba Wizara  kuviendeleza visiwa vidogo  vidogo 48 vilivyopo katika  mkoa wa Kagera  ili  viweze  kuchangia kikamilifu kwenye uchumi.

Akitoa mchango wake Mbunge wa Mafinga (CCM) Mhe. Cosato Chumi amempongeza Waziri Mohamed Mchengerwa na Katibu Mkuu, Hassan Abbasi kwa kazi nzuri waliyofanya wakiwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo amewaomba watumie  michezo katika kuitangaza Tanzania kimataifa.

Aidha, amewashauri kuanzisha miundombinu  mbora kama  viwanja vya michezo  katika maeneo ya Hifadhi kama  taratibu  za kiikolojia  zinaruhusu kufanya hivyo ili wageni wanapotembelea maeneo hayo waweze kupata  burudani ya  michezo mbalimbali.

Amepongeza ubunifu wa Wizara wa kutumia shamba la misitu la Sao Hill la Mafinga mkoani Iringa kutumia  katika mashindano ya kimataifa ya mbio za magari,huku pia akimshukuru Mhe. Rais kwa kutoa fedha ili kuboresha uwanja wa ndege wa Iringa.

Mbunge wa Karatu, Mhe. Daniel Awack ameeleza kuwa Wizara imekuwa ikifanya kazi  kubwa na nzuri  lakini ni muhimu kuwahusisha wananchi  katika  ngazi zote  za uhifadhi  ili kuweza kutatua changamoto zinazojitokeza  badala  ya  Serikali  kwenda  peke yake.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com