METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, June 26, 2023

MWENYEKITI LONDO AITAKA TARURA KUTIMIZA AZMA YA SERIKALI

OR-TAMISEMI, Morogoro

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Dennis Londo ameutaka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuendelea  kuaminika na Serikali kwa  kutekeleza majukumu yake ipasavyo ya kujenga mbiundombinu ya barabara ili kuwaondolea adha ya usafiri wananchi.

Mhe. Londo ametoa kauli hiyo Juni 24, 2023 katika ziara ya kikazi ya kukagua miundombinu ya  barabara zilizojengwa chini ya usimamizi wa TARURA Wilaya ya Morogoro.

Mwenyekiti huyo amesema dhamira ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwaongezea bajeti ya sh.  Bilioni 350 kwa mwaka wa fedha 2023/24 ni kuona umuhimu wa taasisi hiyo  katika kutekeleza majukumu yake hasa katika ujenzi na marekebisho ya barabara maeneo  ya vijijini na mijini ili kuwa na miundombinu rafiki kwa wananchi.

Amesema asilimia kubwa ya watanzania shughuli yao kubwa ni kilimo hivyo TARURA wafanye kazi ili barabara  ziwe rafiki kwa watumiaji na kurahisisha maisha yao.

Mhe.Londo ameipongeza TARURA kujengwa barabara yenye kilometa 70 kwenye Wilaya ya Morogoro ambayo imerahisisha kuunganisha vijiji vinne ikiwamo cha Ngerengere na kuhimiza kutunza miundombinu ya barabara hiyo.

"Kujengwa kwa barabara hii kutawezesha kufika kwa urahisi bwawa la Kidunda ambalo ni mradi mkubwa utakaosaidia upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Morogoro, Pwani na Dar es Salaam,"amesema.

Naye, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Deogratius Ndejembi ameishukuru Kamati hiyo ya Bunge kwa maelekezo yake na kuiahidi TAMISEMI itaendelea kutimiza lengo la Serikali kwa kuisimamia TARURA kutoa huduma bora kwa wananchi.
Share:

Related Posts:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © 2025 WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com