Adolf Jeremiah Mratibu wa Mradi wa YEE Kanda ya Mashariki
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Kibaha.
Halmashauri
ya Wilaya ya Kibaha imewasaidia vijana waliopitia katika mradi wa
kuendeleza Vijana Kiuchumi (YEE) kwa kuwapa jumla ya shilingi milioni 5
kwa ajili ya kuwawezesha kujisajili katika vikundi mbalimbali
vitakavyowasaidia kuendeleza kazi zao.
Msaada
huo umetolewa hivi karibuni baada ya vijana hao kuhitimu mafunzo ya
ufundi yaliyokuwa yakiendeshwa na Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya
Pwani na kutakiwa kuunda vikundi kulingana na fani walizosomea ili
kuweza kujisajili katika vyama hivyo vitakakavyowawezesha kupata fursa
mbalimbali.
Hayo
yamesemwa leo wilayani Kibaha na Afisa Maendeleo ya Vijana wa Wilaya
hiyo, Yahaya Mbogolume alipokuwa akiongea na mwandishi wa habari hii juu
ya maendeleo ya vijana hao baada ya kuhitimu mafunzo ya fani mbalimbali
chini ya mradi huo.
Mbogolume
amesema kuwa mradi huo umekuja wakati muafaka kwani umekuwa chachu ya
maendeleo ya Halmashauri hiyo kwa sababu asilimia kubwa ya wakazi wa
eneo hilo ni vijana ambao walikuwa hawana cha kufanya lakini kupitia
fursa hiyo vijana wameweza kujiajiri.
“Hawa ni
vijana wetu wako kwenye eneo letu hivyo, sisi kama Halmashauri ni wajibu
wetu kuhakikisha wanajiajiri na kuweza kupata kipato , kwa kutambua
hilo tumetoa shilingi milioni 5 kwa ajili ya kusaidia vijana waliopo
kwenye mradi wa YEE kujisajili kwenye vikundi vitakavyowasaidia kuongeza
vipato vyao”, alisema Mbogolume.
Afisa
huyo ameongeza kuwa Halmashauri inaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwapa
mikopo inayowasaidia kuendeleza biashara zao ambapo kwa mwezi huu
halmashauri hiyo imetenga jumla ya shilingi milioni 8 kwa ajili ya
kuwaendeleza kiuchumi vijana hao ambao wameonyesha uhitaji baada ya
kupata mafunzo ya ufundi wa fani mbalimbali.
Kwa
upande wake Mratibu wa Mradi wa YEE Kanda ya Mashariki, Adolf Jeremiah
amesema kuwa mradi huo hautoishia kuwapatia ujuzi tu bali utaendelea
kuwawezesha kichumi ili kuhakikisha vijana hao wanasimama imara na
wanapata maendeleo kupitia fani walizozisomea.
“Shirika
la Plan International tumeamua kusaidia vijana kwa hali na mali hivyo ni
lazima kuhakikisha wanayafikia malengo yao, kwa sasa tumewasiliana na
VETA wafanye tathmini ya vifaa vinavyotakiwa na vijana hao ili tuweze
kuvinunua na kuwagawia waendeleze fani zao zinazowasaidia katika maisha
yao ya kila siku”, alisema Jeremiah.
Naye
mmoja wa wahitimu wa mradi huo, George Geligoali ametoa rai kwa vijana
wenzie kuacha kudharau fursa zinazotolewa na makampuni mbalimbali na
badala yake wazichangamkie kwa kuwa fursa hizo ni kwa ajili ya maendeleo
yao na Taifa kiujumla.
Amelishukuru
Shirika hilo kwa kumuwezesha kupata mafunzo katika fani ya umeme ambayo
inampatia kipato kinachomuwezesha kujikimu yeye na kuhudumia wazazi
wake.
0 comments:
Post a Comment