Na Saida Issa,Dodoma
SERIKALI imesema kuwa inatekeleza Mpango wa Uhifadhi vidakio vya Maji wa mwaka 2021-2035 ambao unahusisha ushirikishwaji wa wadau mbalimbali ikiwemo wananchi.
Hayo yameelezwa Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maji Mhandisi MaryPrica Mahundi alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Kibaha Vijijini Michael Costantino Mwakamo alipouliza Je, Serikali ina mipango gani ya kuliendeleza Bonde la Mto Ruvu kwa kushirikiana na wananchi.
"Kupitia mpango huo, jamii inaelimishwa kuhusu umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji ambapo zimeundwa Jumuiya za Watumia Maji 11 na kupitia Jumuiya hizo, wananchi wanashiriki moja kwa moja kulinda na kutunza rasilimali za maji kwenye maeneo yao,
Vilevile, kupitia mpango huo, Bodi ya Maji ya Bonde la Wami Ruvu inaendelea kujenga miundombinu ya kunyweshea mifugo ili isiendelee kunywa maji kwenye vyanzo vya maji hasa mitoni,"amesema.
Pia amesema kuwa kutafanyika uainishaji wa maeneo ya malisho na vivuko kwa ajili ya mifugo, na kuweka mipango ya pamoja ya matumizi bora ya ardhi hususani kwenye maeneo yanayohusisha vyanzo vya maji.
Aidha, katika kuliendeleza Bonde la
Wami Ruvu, kazi nyingine zinazotekelezwa kupitia mpango huo ni pamoja na
kutambua maeneo ya uhifadhi wa vyanzo, kuyawekea mipaka na kuyatangaza kwenye
Gazeti
la Serikali kuwa maeneo tengefu ambapo hadi sasa maeneo 230 yametambuliwa, 13 yamewekewa mipaka na mawili (2) yametangazwa kwenye Gazeti la Serikali.
0 comments:
Post a Comment