Na WMJJWM, Dodoma
Serikali
imewaagiza Wataalamu wa Mipango na Uratibu katika Sekretarieti za Mikoa kuhakikisha
wanatenga Bajeti za utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na
Maendeleo ya awali ya Mtoto (MMMAM) ili kufanikisha malengo ya uanzishwaji wa
programu hiyo.
Waziri wa
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy
Gwajima ametoa Rai hiyo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya utekelezaji wa
Programu hiyo kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Makatibu Tawala
Wasaidizi wa Mipango na Uratibu wa Sekretarieti za Mikoa na Wadau jijini
Dodoma.
Waziri Dkt.
Gwajima amesema katika bajeti zijazo itabidi uhakiki wa bajeti ufanyike ili
kubaini kama bajeti ya utekelezaji wa Programu hiyo umezingatiwa.
"Baada ya
mafunzo haya Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mipango na Uratibu muende mkatusaidie
kuona namna ambavyo afua za Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto
zitaingizwa kwenye bajeti ya Serikali katika ngazi ya Mikoa na Halmashauri ili
kuimarisha utekelezaji katika ngazi ya msingi" amesema Dkt. Gwajima.
Naye Mkurugenzi
wa Maendeleo ya Jamii Patrick Golwike, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John
Jingu, amebainisha kuwa mafunzo hayo ni muendelezo wa jitihada za Wizara na
Wadau kuhakikisha utekelezaji wenye ufanisi wa programu hiyo.
"Bila
kujenga uelewa kwa watendaji hawataweza kufikia malengo ya programu hii hivyo,
lengo ni kujenga uwezo wa wataalamu
kwenye kutenga bajeti ambapo wataalamu
124 tayari wameshafikiwa, wakiwemo waandishi wa Habari" amesema Golwike.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Shirika la Children in Crossfire, Craig Ferla amesema mara nyingi
kuna changamoto ya utekelezaji wa Programu hasa ngazi za chini hivyo ni faraja
ya pekee kuwa na Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mipango na Uratibu kwenye mafunzo
haya.
"Kwa sensa
ya mwaka huu idadi ya watoto wenye umri wa miaka 0-8 ni 27% ya Watanzania
ambayo ni sawa na watoto milioni 16 hivyo, watoto hawa ni nguvu kazi ya kipekee
ya taifa itakayochagiza uchumi wetu kwa namna tusiyoitarajia" amesema
Ferla.
Naye Katibu
Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu kutoka Mkoa wa Dar es Salaam Chillah Moses
ameishukuru Wizara kwa jitihada zinazofanywa kuhakikisha utengaji wa bajeti ya
kutekeleza programu hiyo kwa manufaa ya watoto nchini.
"Inawezekana
wengi wetu tulikuwa hatulichukulii suala la malezi ya watoto kwa uzito
unaostahili, lakini Serikali na hata Mhe. Rais mwenyewe anathamini watoto,
tunaahidi kuhakikisha bajeti zinapita, safari ya mtoto wa miaka 0-8
inatuhusu".
0 comments:
Post a Comment