METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, May 28, 2023

SERIKALI KUHAKIKISHA WATOTO WOTE WANAPATA HUDUMA ZA MSINGI-WAZIRI GWAJIMA

Na WMJJWM, Dar Es Salaam

Serikali itaendelea kuhakikisha watoto wote wanapata huduma za msingi kupitia vituo vya kulea watoto nchi nzima kwa kushirikiana na wadau wote.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameyasema hayo wakati wa hafla ya "Gusa Moyo wa Watoto" , iliyoandaliwa na Ubalozi wa Jamhuri ya watu wa China, katika kituo cha kulea watoto cha Ijango Zaidia Orphanage, Sinza Wilaya ya Ubungo mkoa wa Dar es Salaam Mei 28, 2023.

Waziri Dkt. Gwajima amesema amefarijika na mpango mzuri uliofanywa na mke wa Rais wa China kugusa mioyo ya watoto wa Kitanzania.

"Kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan napenda kusema Wizara hii inaungana na maono haya ya wenza wanawake wa Marais na kuyashusha nchi nzima, tutaratibu mfumo mzima kwa kila anayeguswa kuwasaidia Yatima popote alipo kujua anapita njia gani kuwafikia watoto wote" amesema Waziri Dkt. Gwajima.

Akizungumza pia kwa niaba ya Mke wa Rais wa Zanzibar na mwanzilishi Taasisi ya Maisha Bora Zanzibar Mhe. Mama Mariam Mwinyi, Waziri Dkt. Gwajima ametoa rai kwa Wadau kuuenzi mpango huo ulioanzishwa na Mke wa Rais wa China Mhe. Profesa Peng Liyuan na kuufanya  kuwa endelevu.

"Lengo la mpango huu ni kusaidia watoto waliokosa fursa barani Afrika kuwa na maisha bora ya baadaye" amesema Dkt. Gwajima.

Kwa upande wake Balozi wa China nchini Tanzania mhe. Chen Mingjian  amesema katika kuadhimisha miaka 60 ya ushirikiano wa Madaktari wa China na Serikali ya Tanzania Jamhuri ya watu wa China imetoa mahitai mbalimbali ili kusaidia maisha bora kwa watoto wa Kitanzania.

Ameongeza kwamba kupitia ushirikiano huo, tayari wagonjwa 20 elfu wa Kitanzania wametibiwa kwa China kuongeza nguvu katika eneo la wataalamu na Hospitali.

Awali akizungumza katika tukio hilo, mmiliki wa kitio cha Zaidia Orphanage, Zaidia Hassan amebainisha kuwa kituo hicho kina watoto 52 hadi sasa ambapo  kimeshafanikiwa kuwaunganisha watoto 80 na familia zao.

"Tunawaandaa watoto wetu kisaikolojia kuanzia miaka 14 kuwa wakishafikisha umri wa miaka 18 wanatakiwa kutoka kwenye kituo, baadhi yao wamesoma na wanajitgemea" amesema Zaidia.

Ameishukuru pia Serikali kwa ushirikiano katika vituo vya kulea watoto kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii.

Katika tukio hilo, Waziri Gwajima amekabidhi mahitaji mbalimbali kwa ajili ya watoto ikiwemo vifaa vya masomo  na vya michezo.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com