METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, May 27, 2023

MADIWANI WA BARIADI WAKIONGOZA NA MBUNGE ENG KUNDO WAFANYA KIKAO KAZI NA NAIBU WAZIRI MARY MASANJA


Na Mathias Canal, Dodoma

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu jana tarehe 26 Mei 2023 wamekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe Mary Masanja Ofisini kwake Jijini Dodoma.

Katika kikao hicho kilichohudhuriwa pia na Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mhe Mhandisi Mathew Kundo ambaye ni Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, madiwani hao waliwasilisha changamoto mbalimbali ikiwemo kuvamiwa na tembo kwa Wananchi wanaoishi pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa  ya Serengeti, Mapori ya Akiba ya Maswa, Kijereshi na Mwiba.

Changamoto zingine walizowasilisha mbele ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii ni pamoja na kutokuwa na kituo cha askari wa wanyamapori, kutopewa fedha za uwajibikaji kwa jamii (CSR) pamoja na malalamiko ya kutokuwa na Mahusiano mazuri baina ya askari wa uhifadhi na wananchi.

Kwa kauli moja madiwani hao wameiomba serikali kuhakikisha kuwa askari wa wanyamapori wanakuwa karibu na wananchi, wawe wanapatiwa CSR, wajengewe kituo cha askari wa uhifadhi, pamoja na askari wa uhifadhi kuchukua hatua haraka mara  inapotokea tembo kuvamia makazi ya wananchi.

Pia madiwani hao wameomba kutafsiriwa mipaka ya Hifadhi na viwekwe vigingi ambavyo vinaonekana ili wananchi wasiingie eneo la hifadhi.

Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe Mary Masanja ametoa maelekezo kujengwa kituo, pia CSR zitolewe, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa wanatoa elimu kwa wananchi namna ya kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu hususani tembo ikiwa ni pamoja na askari hao kuwa na Mahusiano mazuri na wananchi.

Pia Naibu Waziri Mhe Masanja amelielekeza Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kutembelea eneo hilo kwa ajili ya kutafsiri mipaka kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji na pia kuwekwa vigingi virefu vinavyoonekana.

Kadhalika, Mhe Masanja amewataka Madiwani kuzungumza na wananchi katika mikutano yao ya hadhara na kuwaambia ukweli kwamba hawatakiwi kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo ya hifadhi.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com