METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, April 5, 2023

JUMLA YA WATU 805 GEREZA LA BUKOBA WAFIKIWA NA ELIMU YA TAHADHARI NA KUJIKINGA NA MARBURG

Lango kuu la Gereza la Bukoba Mkoani Kagera.

Mmoja wa Maafisa gereza la Bukoba akipokea bango la uelimishaji kuhusu ugonjwa wa Marburg.                                                                     
image.png


Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Beauty Mwambebule akitoa elimu jinsi ya kujikinga na Marburg katika gereza la Bukoba mkoani Kagera.


Mmoja wa Maaskari magereza ,gereza la Bukoba akizingatia kanuni  za afya kwa kunawa mikono kwa maji tiririka .

Mtaalam wa Afya kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera Jackline Saulo 

Na.Elimu ya Afya kwa Umma.

Jumla ya watu 805  wakiwemo wafungwa, watumishi wa magereza pamoja na familia zao   katika Gereza la Bukoba  Mkoani Kagera  wamefikiwa na elimu ya kujikinga na Ugonjwa wa Marburg .

 

Akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Afya kwa Umma, Idara ya Kinga, Wizara ya Afya Dkt.Tumaini Haonga baada ya kutembelea gerezani hapo  kutoa elimu namna ya kujikinga na  ugonjwa wa Marburg, Beauty Mwambebule amesema Marburg ni muhimu kuchukua tahadhari mapema juu ya ugonjwa huo.


“Kinga ni bora kuliko tiba ; wakati mwingine  inaweza kuchukua kuanzia siku 2 hadi 21 kuonesha dalili mfano homa, kutapika, kuharisha damu au kutapika damu ni muhimu tuchukue tahadhari mapema” amesema Beauty Mwambebule, Mwakilishi wa Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Wizara ya Afya.

Kwa upande wake Mtaalam wa Afya kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera Jackline Saulo amesema ni muhimu kwa kila  mtu kuepuka misongamano isiyo ya lazima ambapo pia maelekezo yameshatolewa kuhakikisha sehemu zote zenye mikusanyiko ya watu panakuwepo na vifaa maalum vya kunawia mikono.

Wakitoa neno la shukrani baadhi ya watumishi wa Gereza la Bukoba akiwemo Mkaguzi wa Jeshi la Magereza Fredrck Katabazi  huku Mkaguzi Msaidizi Venance Vedastus  ambaye ni afisa mapokezi gereza la Bukoba  wametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa kuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mara tu yanaporipotiwa hasa kwa kuongeza wigo wa uelimishaji.

Pia katika gereza la Bukoba yametolewa mabango yenye ujumbe mahsusi kuhusu elimu ya kujikinga na Ugonjwa wa Marburg , dalili zake na jinsi unavyoenezwa.

Ikumbuke kuwa watalaam wa Afya  kutoka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Mkoa wa Kagera wameendelea kutoa elimu jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa Marburg  katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kagera kwa kufikia makundi mbalimbali ikiwemo magereza, viongozi wa dini, waendesha pikipiki, maduka na sehemu zote za kutolea huduma na sehemu zenye mikusanyiko.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com