METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, March 21, 2023

RAS DKT MGANGA AWAKATAA WATUMISHI WAPIGA MAJUNGU SINGIDA, ASISITIZA USHIRIKIANO KATIKA KUWATUMIKIA WANANCHI

Aliyekuwa Katibu Tawala Mkoa wa Singida ambaye amestaafu Mwl Dorothy Mwaluko(Kulia) akimkabidhi Nyaraka Katibu Tawala Mpya  Dkt Fatma Mganga mapemba leo Machi 21, 2023. 

(Wakwanza Kushoto)Dkt. Fatma Mganga Katibu Tawala Mkoa wa Singida, (Katikati) Peter Serukamba Mkuu Mkoa wa Singida na (Kulia) Mwl. Dorothy Mwaluko Katibu Tawala Aliyestaafu wakiwa katika hafla ya makabidhio ya ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida hii leo machi 21, 2023. 

Katibu Tawala Mpya wa Mkoa wa Singida Akizungumza na watumishi wa Mkoa wa Singida 

Watumishi wa Mkoa wa Singida wakifuatilia Hafla ya makabidhiano  ya ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida. 


Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba Akizungumza kwenye hafla hiyo.

Issa Nassor Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Singida Akizungumza kabla ya kusoma dua wakati wa makabidhiano ya ofisi ya Katibu Tawala wa  Mkoa wa Singida.

Makabidhiano yakiendelea.

Na Hamis Hussein - Singida

KATIBU Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Fatma Mganga amewataka watumishi wote mkoani hapa kutoa ushirikiano na kuacha majungu na kwamba hatamvumilia mtumishi yeyote atakayekuwa na majungu mahala pa kazi.

Dkt. Mganga amesema hayo leo Machi 21, 2023  wakati akizungumza na watumishi na wakuu wa idara wa Mkoa wa Singida  baada ya kukabidhiwa ofisi na aliyekuwa  Katibu Tawala  mkoani hapa ambaye amestaafu Mwl. Dorothy.

Dkt. Mganga ambaye awali alikuwa katibu tawala Mkoa wa Dodoma amesema Majungu kwa watumishi wa umma mahala pakazi yanasababisha migongano na kupelekea kukwamisha utendaji na kushindwa kutimiza malengo hivyo akasisitiza kuwepo kwa ushikiano katika kutimiza malengo ya serikali ya kuwahudumia wananchi.

“Mimi nitakuwa tayari kupokea maoni lakini sitakuwa tayari kupokea majungu, sidhani kama ukija ukaniambia ‘unajua Grace kazi yake ni hivi, yule hafai hata kidogo’ mimi nitakuuliza je wewe na yeye mkoje? Ili ukamilishe hadithi nzima, kwa sababu majungu mahala pakazi huwa yanaleta migongano na mwisho wa siku huwa tunashindwa kufikia malengo ambayo tumeelekezwa kwahiyo sitapenda majungu lakini nakaribisha maoni” alisema Dkt Mganga.

RAS Dkt Mganga aliongeza kwa kuwataka watumishi hao kushirikiana katika kuwatumikia wananchi ambao ndio wanafanya wawepo katika nafasi walizonazo badala ya kuwaona wanawapotezea muda.

“Mimi pekee yangu sitaweza lakini tukishirkiane kwa pamoja ninaamini tutakwenda kufanya mambo makubwa katika Mkoa wa Singida,Dorothy alifanya vizuri sana na mimi ninaomba ushirikiano ili tukaboreshe pale ambapo Dorothy alisukumba basi sisi tuliobakia tuendelee tokea pale, Lakini niwaombe kutenda kazi kwa bidii, wananchi ndio waajiri wetu twendeni tukawatumikie watu wa Singida tusiwaone kama wanatupotezea muda” Aliongeza Dkt Mganga.

Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba alimshukuru Katibu Tawala  ambaye amestaaafu Mwl. Dorothy Mwaluko katika utendaji wake ambapo pamoja na mambo mengine alifanikisha maendeleo mengi katika nyaja mbalimbali za Mkoa huu hivyo akatumia nafasi hiyo kumshukuru kwa utumishi wake na kwamba alimrahisishia  utendaji wake kazi wa Ukuu wa Mkoa.

RC Serukamba aliongeza kwa kuwataka watumishi wa Mkoa wa Singida kutekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja kufatilia na kuielelewa miradi inayotekelezwa hasa ngazi za hamalshauri ambapo amewaonya baadhi ya watumishi  hao kuwa waongo pindi wanapoulizwa kuhusu mambo wanayoyasimamia.

“Kwenye halmashuri kugumu bado watu wanacapacity ya kusema uongo, mtu wa halmashauri ukimuliza jambo jibu jiulize mara mbili, kuna chance anakudanganya lakini sasa tumepata RAS aliyeanzia kwenye halmashauri  hivyo anawajua, kwahiyo uongo mliokuwa mnaniambia mimi msipeleke huko maisha yenu yatakuwa magumu sana, wengi wenu  hamfanyi kazi kwa bidii, nyie mnatuma na yule mliomtuma naye anatuma matokea  yake vitu vinakuwa haviko kwenye mikono yenu kwahiyo ni rahisi watu wote tukawa tumedanganywa” Alisema RC Serukamba.

Naye aliyekuwa Katibu Tawala Mkoa wa Singida ambaye amestaafu Mwl. Dorothy Mwaluko amewashukuru watumishi wote wa Mkoa wa Singida kwa ushirikiano wao katika mambo mbalimbali ya kiutendaji ambayo yameleta chachu ya maendeleo kwa wananchi huku akiwataka watumishi hao kuendelea kuwatumika wananchi wa mkoa wa Singida  ili kutimiza malengo yaliyowekwa na Serikali.

Mwl. Mwaluko alisisitiza watumishi kuwajibika katika utatuzi wa changamoto za wananchi wa Singida ambapo amesema utashi wao katika kutumikia wananchi kwa kufuata taratibu za utumishi wa umma utasaidia katika kutimiza malengo ya serikali ya kutatua changamoto za wananchi.

 

 

 

 

 

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com