Wenyeviti wa Halmashauri za Mkoa wa Singida wakiwa kwenye kikao cha Ushauri cha Mkoa RCC kikao hicho kimefanyika Jumamosi Machi 11, 2023 katika ukumbi wa Mikutano wa Mkoa wa Singida. |
Mkuu wa Mkoa wa Peter Serukamba akizungumzia suala la ugawaji mbegu za ruzuku za alizeti kwenye kikao cha RCC juzi Machi 11, 2023. |
Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda akichangia hoja juu ya ugawaji wa Mbegu za Ruzuku za Alizeti kwa wakulima.kwenye kikao cha RCC mkoa wa Singida. |
Wajumbe wa Kikao cha Ushauri cha Mkoa RCC wakifuatilia taarifa mbalimbali kwenye Mawalisho. |
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Innocent Msengi akichangia Hoja kwenye Kikao cha RCC Mkoa wa Singida. |
|
Katibu Tawala anayesimamia Maendeleo ya Kilimo na Uchumi Mkoa wa Singida Stanslaus Choaji akisoma ripoti kuhusu utekelezaji wa shughuli za Kilimo ikiwemo mazao ya Kimkakati. |
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida Jeshi Lupembe akichangia hoja kwenye Kikao cha RCC Mkoa wa Singida. |
Na Hamis Hussein - Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida Peter
Serukamba ameziagiza Halmashauri zote mkoani humo kuongeza kasi ya kugawa mbegu
za rukuzu za alizeti kwa wakulima kabla ya msimu haujamalizika ili kutimiza
lengo la Mkoa la kulima Ekari laki 631391 mwaka huu vinginevyo zitatakiwa
kuzilipia Mbegu hizo kwa wakala wa Mbegu za Kilimo ASA.
RC Serukamba ametoa agizo hilo Jumamosi Machi 11, 2023 kwa halmashauri baada ya kuwasilishwa kwa ripoti ya kilimo ya Mkoa kwenye kikao
cha ushauri RCC, ambapo ripoti hiyo imeonyesha kuwa bado tani 101.799 kati ya
tani 395.38 hazijawafikia wakulima hivyo mkuu huyo akatumia wasaa huo kumwagiza
Katibu Tawala anayesimamia eneo la Kilimo na Uchumi Stanslausi Choaji
kufuatilia ugawaji wa mbegu hizo.
Serukamba alisema kuwa
Halmashauri zitakazoshindwa kuzigawa mbegu zilizosalia kwa wakulima zitatakiwa
kuwalipa fedha wakala wa mbegu za kilimo ASA kufidia mbegu ambazo
hazitachukuliwa na wakulima.
“Unajua Wizara ya kilimo imetupendelea sisi juzi amenipigia Waziri ananiambia
‘Peter hivi kweli nasikia kuna watu hawajagawa mbegu?’ na nikiwaangalia sababu
zenu wala hakuna anayesikitika simply because hulimi wewe sasa zile halmashauri
ambazo haziwezi kugawa na mnaona kuna halmashauri inaweza kugawa zipelekeni
huko lakini wale ambao hawawezi kuzisambaza Walipe fedha za ASA” alisema RC
Serukamba.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Singida
alionyeshwa kutofurahishwa kwenye kikao hicho kilichofanya Jumamosi ya Machi 11
na amemwagiza Katibu Tawala anayesimamia Maendeleo ya Kilimo na Uchumi kuzifuatilia Halmashauri hizo kujiridhisha na
zoezi hilo la Ugawaji wa mbegu na kusema
kuwa endapo halmashauri itashindwa kugawa mbegu hizo kwa muda uliobakia
zitanyang’anywa hatimaye zitalazimika kulipa fedha kwa Wakala wa Mbegu za
Kilimo.
Aliongeza kwa kuwasisitiza
viongozi wa Mkoa wa Singida kutoka maofisini na kwenda kuwasikiliza na kutatua
kero za wananchi badala ya kuwa na ubinafsi ambao unarudisha nyumba maendeleo
kwa wananchi.
“Tutaonekana watu wa ajabu tusiosaidia watu, hii Level ya ubinafsi imezidi haiwezekani, tusikaeni maofisi jamani hapa ni kwamba nyie mkishawapelekea watendaji wa vijiji kazi yako imeisha mtendaji amefanya you don’t care, ndio style yetu na inawezekana kuna Wakurugenzi, Wenyeviti wa halmashauri hapa kwenye hii ripoti walikuwa hawajui kama mbegu hazijagawanywa”Aliongeza RC Serukamba.
Awali Akisoma Ripoti hiyo ya Kilimo mwishoni mwa Juma lililopita Katibu Tawala wa Maendeleo ya Kilimo na Uchumi Stanslaus Choaji amesema hadi kufikia mwezi Februari Mwaka huu Mkoa ulikuwa umetekeleza asilimi 75.9% kwa kulima Ekari 479855.75 za zao la alizeti ambapo Mkoa umepokea mbegu za ruzuku za alizeti aina ya Record tani 395.38 na tayari tani 293.581 zimewafikia wakulima.
Choaji alisema katika ekari
zilizolimwa hadi sasa endapo hali ya hewa ikiendelea vizuri mkoa utaweza kuvuna
tani 317297.2 sawa na asilimia 64.4 % kati ya lengo la kupata tani 492486 kwa
Msimu huu wa kilimo.
Suleiman Mwenda Mkuu wa Wilaya ya
Iramba akizungumza kwenye kikao hicho akachangia juu ya ugawaji wa mbegu hizo
ambapo amesema hivi karibu alifanya mkutano na wananchi wa Mgongo na Shelui ambapo Mkulima alilalamika kukosa mbegu hizo za ruzuku akidai kuwa wakulima wamekuwa wakitakiwa kulipia fedha Taslimu badala ya kukopeshwa kama
ilivyoelekeza serikali.
Baadhi ya Wenyeviti wa halmashauri
wametaja changamoto zilizopelekea kushindwa kugawa mbegu zilizo salia kwa
wakulima sababu hizo ikiwa pamoja na hali ya hewa kubadilika ambapo mvua kukatika jambo lililopelekea
wakulima kushindwa kulima.
0 comments:
Post a Comment