KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imekiagiza Chuo cha Viwanda vya Mazao ya Misitu (FITI) kuunda kitengo cha uongezaji thamani wa Mazao ya Misitu ili kuondokana na uagizaji wa bidhaa za samani kutoka nchi za nje.
Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava
ameyasema hayo Machi 17, 2023 wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Chuo cha
Viwanda vya Mazao ya Misitu (FITI) Mjini Moshi.
“Bado tuna
tatizo kubwa kwenye uongezaji wa thamani wa Mazao ya Misitu inayosababisha
uingizwaji wa bidhaa za Samani hasa kutoka China kuwa mkubwa hivyo naagiza
Menejimenti mkaangalie namna ya kuunda kitengo cha uongezaji thamani Mazao ya
Misitu ili tuondokane na changamoto hii” Mhe. Mnzava amesisitiza.
Aidha, ameutaka
Uongozi wa Chuo hicho kuendelea kuwafundisha vijana wa Kitanzania teknolojia na
ujuzi wa uzalishaji wa bidhaa za Samani za kisasa unaoendana na mazingira ya
sasa ili kupunguza kasumba ya uingizaji wa bidhaa kutoka nje na pia kutengeneza
ajira kwa vijana.
Mhe. Mnzava
amekiagiza chuo hicho kuendelea kufanya biashara, kutafuta miradi mipya na
kutengeneza maandiko ili kuwa na njia mbadala za kujiongezea mapato.
Kwa upande wake
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amesema mpango wa
Serikali ni kuangalia namna ya kukabiliana na ushindani wa soko la nje kwa
kutengeneza bidhaa kwa kutumia teknolojia inayotumika nje ili kupunguza kasumba
ya watu kukimbilia bidhaa za China.
Aidha, amesema
chuo hicho kitaendelea kufundisha vijana ili ifike mahala ambapo mwanafunzi
akitoka nje anaweza kuingia kwenye ushindani wa soko la nje.
Chuo cha Viwanda
vya Misitu kilianzishwa mwaka 1976 kwa msaada wa Serikali ya Sweden kupitia
shirika lake la maendeleo la SIDA kwa madhumuni ya kutoa mafunzo ya viwanda vya
misitu .
0 comments:
Post a Comment