METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, March 18, 2023

FITI YATAKIWA KUONGEZA THAMANI YA BIDHAA ZA MAZAO YA MISITU ILI KUPUNGUZA UAGIZAJI BIDHAA KUTOKA NJE








KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imekiagiza Chuo cha Viwanda vya Mazao ya Misitu (FITI) kuunda kitengo cha uongezaji thamani wa Mazao ya Misitu ili kuondokana na uagizaji wa bidhaa za samani kutoka nchi za nje.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava ameyasema hayo Machi 17, 2023 wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Chuo cha Viwanda vya Mazao ya Misitu (FITI) Mjini Moshi.

“Bado tuna tatizo kubwa kwenye uongezaji wa thamani wa Mazao ya Misitu inayosababisha uingizwaji wa bidhaa za Samani hasa kutoka China kuwa mkubwa hivyo naagiza Menejimenti mkaangalie namna ya kuunda kitengo cha uongezaji thamani Mazao ya Misitu ili tuondokane na changamoto hii” Mhe. Mnzava amesisitiza.

Aidha, ameutaka Uongozi wa Chuo hicho kuendelea kuwafundisha vijana wa Kitanzania teknolojia na ujuzi wa uzalishaji wa bidhaa za Samani za kisasa unaoendana na mazingira ya sasa ili kupunguza kasumba ya uingizaji wa bidhaa kutoka nje na pia  kutengeneza  ajira kwa vijana.

Mhe. Mnzava amekiagiza chuo hicho kuendelea kufanya biashara, kutafuta miradi mipya na kutengeneza maandiko ili kuwa na njia mbadala za kujiongezea mapato.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amesema mpango wa Serikali ni kuangalia namna ya kukabiliana na ushindani wa soko la nje kwa kutengeneza bidhaa kwa kutumia teknolojia inayotumika nje ili kupunguza kasumba ya watu kukimbilia bidhaa za China.

Aidha, amesema chuo hicho kitaendelea kufundisha vijana ili ifike mahala ambapo mwanafunzi akitoka nje anaweza kuingia kwenye ushindani wa soko la nje.

Chuo cha Viwanda vya Misitu kilianzishwa mwaka 1976 kwa msaada wa Serikali ya Sweden kupitia shirika lake la maendeleo la SIDA kwa madhumuni ya kutoa mafunzo ya viwanda vya misitu .

 

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com