METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, March 1, 2023

CHONGOLO AENDELEA KUHIMIZA UMUHIMU WA UFUNDI KWA VIJANA NA KADA NYINGINE

Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati Dodoma, John Mwanja akitoa taarifa kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo (wa pili kushoto) kuhusu ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Veta Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea miradi ya maendeleo aliyoifanya Februari 28, 2023. 

Na Dotto Mwaibale,Ikungi

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo,akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani hapa  ameendelea kuhimiza vijana kujiunga na vyuo vya ufundi ili kupata mafunzo ya ufundi yatakayo wasaidia kupata ajira pamoja na kujiajiri.

Akiwa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo  alipokitembelea Chuo cha Ufundi Stadi cha Veta wilayani Ikungi mkoani Singida Februari 28, 2023 aliitaka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kuanza kutoa elimu ya ufundi kuanzia ngazi ya chini na kueleza umuhimu wake jambo litakalosaidia kuwavutia vijana wengi.

Chongolo alisema mbali ya vijana kupata elimu hiyo aliiomba mamlaka hiyo somo la kompyuta liwe la kawaida na la muhimu ili kila mwanafunzi alifahamu kwani hivi sasa mambo mengi ya teknolia ya ufundi yanahusisha matumizi ya kompyuta.

“Matumizi ya kompyuta yawe ya lazima katika mafunzo ya ufundi kuanzia ngazi ya chini kutokana na umuhimu wake na kukua kwa teknolojia” alisema Chongolo.

Chongolo aliiomba Veta kuanza kutoa mafunzo hayo ya ufundi kuanzia shule za sekondari lengo likiwa ni kuwaanda kujua umuhimu wa ufundi na faida zake.

Alisema lengo la Serikali ni kujenga vyuo vya Veta katika kila wilaya hapa nchini ambapo katika miaka mitatu mfululizo imekuwa ikitoa mafunzo ya ufundi bure na akaiomba Veta kujikita zaidi katika uhamasishaji wa vijana kujiunga katika vyuo hivyo.

Aidha Chongolo alihimiza  kila mtu kujifunza walau fani moja ya ufundi bila kujali elimu aliyonayo ambayo haimzuii mtu kuwa na ujuzi mwingine akijitolea mfano yeye ambaye ni fundi mahiri wa kuchomelea vyuma lakini leo hii ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)

Chongolo alisema hivi sasa wapo vijana wengi hawana elimu ya ufundi na wengi wana elimu ya juu hivyo ni muhimu kutengeneza msingi kuanzia shule za sekondari.

 Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati,John Mwanja, alisema ujenzi wa chuo cha VETA Ikungi ulianza katika bajeti ya 2019/2020 ambapo hadi sasa Sh.bilioni 2.3 zimeshatumika katika ujenzi huo ambao utakamilika Aprili mwaka huu.

Mwanja alisema Serikali imetoa Sh.milioni 259 ili kukamilisha ujenzi wa chuo hicho na kwamba kitaanza kutoa mafunzo ya kozi ndefu kwa wanafunzi 240 na wa kozi fupi kati wanafunzi 250 hadi 900 kwa mwaka.

Alisema faida ya chuo hicho mara kitakapokamilika kinatarajiwa kuhudumia wakazi wapatao 343,985 wa Wilaya ya Ikungi na wakazi wapatao  1,754,370  wa Mkoa  wa  Singida.

 

Alisema katika kutekeleza mradi huo VETA imekumbana na changamoto mbali mbali kama kupanda  kwa bei  ya  vifaa vya  ujenzi  wakati wakiendelea  na  utekelezaji
wa  mradi,  hali iliyopelekea  pesa iliyotengwa  kutokidhi  mahitaji
halisi  ya  mradi kutokana  na  bei za  vifaa kupanda zaidi ya
matarajio ya awali.

.

Alitaja changamoto nyingine waliyokumbana nayo ni uwezo mdogo wa kiuchumi wa mafundi waliowatumia hivyo kupelekea kushindwa kuwalipa vibarua wao kwa wakati na kupelekea baadhi yao kuacha kazi, hivyo kupelekea kuchelewa kwa utekelezaji wa mradi.

 

Mwanja alitumia nafasi hiyo kutoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha mafunzo ya ufundi stadi nchini kwa kutoa fedha za miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vyuo vipya vya Veta na uboreshaji wa vyuo vya zamani.

Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati Dodoma, John Mwanja akimuelekeza jambo Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo (wa tatu kushoto) wakati wa ziara hiyo ya kutembelea Chuo cha Veta Ikungi.
Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa VETA, Felix Staki, ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa VETA, akizungumza jambo na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo (wa pili kushoto) wakati wa ziara hiyo.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo (katikati) akifurahia jambo na Mwandishi Thobias Mwanakatwe wakati wa ziara hiyo ya kutembelea Chuo cha Ufundi Stadi Veta Wilaya ya Ikungi.
Muonekano wa baadhi ya majengo ya Chuo cha Ufundi Veta Wilaya ya Ikungi.
Muonekano wa baadhi ya majengo ya Chuo cha Ufundi Veta Wilaya ya Ikungi.

Muonekano wa baadhi ya samani katika moja ya  chumba ya Chuo cha Ufundi Veta Wilaya ya Ikungi.

 Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo (katikati) akiwa na viongozi wengine wakati akitoka kukagua jengo la Karakana ya magari katika chuo hicho.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com