METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, March 17, 2023

BARAZA LA MADIWANI MKALAMA LAMFUTA KAZI MTUMISHI MTORO ASIYEWAJIBIKA, WENGINE WAWILI WAPEWA ONYO NA ADHABU

 

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama likiwa  kwenye kikao cha Robo ya Pili ya Mwaka kikao kilichofanyika ukumbi wa Halmashauri hapo jana Machi 16, 2023.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Asia Messos Akizungumza wakati wa Baraza la Madiwani jana.

Diwani wa Vitimaalum  Kata ya Nkinto Florence Yona akiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mkalama.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama James Mkwega  kushoto  na Mkurugenzi  wa Halmashauri hiyo Asia Messos wakiwa kwenye picha  pamoja wakati Kikao kikiendelea.


Madiwani na waalikwa mbalimbali wakiwa katika kikao hicho.

Kikao cha baraza la Madiwani kikiendelea.

Wakuu wa idara na Watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama wakiwa kwenye Kikoa cha Baraza la Madiwani kilichoketi jana Machi 16, 2o23.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama James Mkwega akifunga kikao cha Baraza la Madiwani hapo jana.


Na Hamis Hussein - Mkalama

BARAZA  la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama limemfuta kazi Mtumishi mmoja huku wengine wawili wakipewa onyo na adhabu mbalimbali kutokana na watumishi hao kukiuka taratibu na Kanuni za kiutendaji za utumishi wa Umma.

Baraza hilo ambalo limeketi jana Machi 16, 2023 limepitisha maazimio hayo kwa watumishi hao wa umma baada ya kupokea malalamiko yanayowakabili watumishi wale ambapo kamati ya utumishi wa umma imekubaliana kuchukua hatua hizo.

Mtumishi ambaye amefukuwa ni Elibarick Siasi Ombai ambaye alikuwa mtendaji wa Kijiji cha Maziliga ambapo kamati imemfuta kazi kutokana na kushindwa kusimamia majukumu yake na hali ya utoro uliopitiliza.

Mtumishi Mwingine ni Afisa Elimu Vielelezo wa Halamshauri  hiyo Nasibu Mohamed Pangaela ambapo amepewa adhabu ya kushushwa cheo na kubadilishiwa kituo cha kazi wakati akiwa kwenye matatazamio kutokana na utoro kazini.

Na Mtumishi wa Mwisho ni Nkwangu Musa Nkwangu Aliyekuwa Mtendaji wa Kijiji cha Kidarafa ambaye kwa sasa yupo kijiji cha Msiu, yeye amepewa miezi mitatu kurudisha shilingi 601,000/= fedha mbichi ambapo mtendaji huyo hakuzipeleka benki fedha hizo na kuzitumia kwa matumizi yake mwenyewe.

Baadaya kutoa taarifa ya hatua za kinidhamu kwa watumishi hao watatu, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama James Mkwega amewataka watendaji wa halmashauri hiyo kutekeleza wajibu wao ambapo amewasisitiza wakuu wa idara kuwaka ratiba za kufanikisha majukumu yao kwa ufanisi.

“Watendaji Wangu niwaombe sana mjipange kila mmoja kwa nafasi yake sio lazima tukupe azimio ndio ufanye kazi, tunatamani kuona kila mkuu wa idara anapanga ratiba yake ya kazi ili ilete ufanisi yaani siku moja baraza hili tuligeuzi liwe la kutoa hongera na pongezi kwa kila Mkuu wa idara kwamba mmefanya Vizuri, kwahiyo natamani kuona hivyo sio lazima tuwe na Maazimio mengi kama kazi inaenda vizuri” alisema Mkwega.

Kuhusu kupunguza hoja za ukaguzi Mwenyekiti huyo alisisitiza watendaji hao kupitia kamati ya fedha kushirikiana ili hoja hizo ziwe zimeisha ifikapo robo nyingine Mwaka.

“Kwenye kamati yetu ya Fedha suala la hoja za ukaguzi tumelitolea muda, yale yanayowezekana kufuta hizo hoja zifutwe kila mmoja kwa nafasi yake hatupendi kuendelea tena kwenye Quarter inayokuja tukutane na hoja hizo hizo bado zimesimama zilivyo, kila mmoja apambane aone namna anavyoweza kufuta hoja yake” aliongeza Mkwega.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Asia Messos amewaeleza Madiwani na watendaji wengine kuhamisha wakulima kuchukua mbegu za  ruzuku za serikali ili walime katika kipindi hiki ambacho mvua imerejea ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Mkuu wa Mkoa aliyeagizwa Wakulima kugawiwa mbegu hizo kwa Mkopo.

Aidha kuhusu ujenzi wa miundombinu ya vyoo katika shule za Chemchem na Miganga Mkurugenzi huyo alisema kuwa tayari ameshakaa na wakuu wa shule pamoja na watendaji kuona namna ya kujenga vyoo hivyo hivyo akatumia baraza hilo kuwaomba Madiwani kuhamasisha wananchi wao kujitolea nguvu zao kukamilisha miundombinu hiyo ili kuwaweka wanafunzi katika mazingira ya usalama.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com