Na Mathias Canal, Dodoma
Ili kuwezesha upatikanaji wa huduma za ukadiriaji kodi kwa wakati serikali imeagiza Ofisi zote za ardhi nchini kutoa huduma siku zote za juma hadi mwisho wa mwezi aprili.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt. Angeline Mabula ametoa agizo hilo leo tarehe 7 Februari 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma.
Waziri Mabula amewataka wananchi kuendelea kutumia njia za ki-elekroniki ambazo pia zimeanza kutolewa na Benki washirika za CRDB na NMB katika kukadiria na kulipa kodi.
Waziri Mabula amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan ameongeza muda wa msamaha wa riba ya malimbikizo hivyo wananchi wanapaswa kuchangamkia msamaa huo.
Dkt. Mabula amesema kuwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imejipanga kuwahudumia kikamilifu ili kuwawezesha wananchi kupata nafuu ya msamaha wa riba ya kodi ya pago la ardhi iliyotolewa na Mhe. Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani.
Amesisitiza kuwa wananchi, mashirika na kampuni ambazo hazita tumia fursa hiyo Wizara imejipanga kuchukuwa hatua za kisheria kukusanya kodi pamoja na malimbikizo.
Waziri Mabula amezitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na ubatilisho wa milki, kuwafikisha mahakamani kukamata mali na kunadi ili kufidia kodi husika.
“Hivyo, Natoa rai kwa taasisi na mashirika ya umma na wananchi wote kutumia muda uliotolewa hadi April 30 na Mhe. Rais kunufaika na msamaha wa riba uliotolewa na Serikali kulipa deni la msingi (principal amount) ili wasamehewe riba ya malimbikizo ya kodi ya pango la ardhi” Amekaririwa Mhe Mabula
Uamuzi huo wa kuongeza muda umefikiwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo maombi mengi ya wananchi na taasisi yaliyoifikia Serikali.
Waziri Mabula amesema kuwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai hadi Disemba 2022, Wizara imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 90.9 sawa na asilimia 75 ya lengo la makusanyo ya Shilingi Bilioni 121.
“Makusanyo kwa mwaka wa fedha 2022/23 yameongezeka kwa Shilingi bilioni 33.9 ikilinganishwa na kipindi kama hiki kwa mwaka wa Fedha 2021/22” Amesema Mhe Mabula
Dkt Mabula amesema kuwa wananchi 6,211 wamenufaika na msamaha wa riba ya malimbikizo sawa na shilingi 11,931,537,409.80.
“Serikali inaamini kuwa fedha hizo zilizosamehewa zimeenda kuleta nafuu kwa wahusika na kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii nchini” Amesema
Waziri Mabula amemshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt Samia Suluhu Hassani kwa uamuzi wake wa kusamehe kiasi kikubwa hicho kwa lengo la kuwaondolea mzigo wa madeni wananchi na taasisi mbalimbali.
Katika Mwaka wa Fedha 2022/23, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassani alitoa msamaha wa riba ya malimbikizo ya pango la ardhi ambapo wananchi walio na malimbikizo walipewa nafuu ya kulipa deni la msingi ili wasamehewe riba ya malimbikizo kuanzia Julai hadi Disemba, 2022
MWISHO
0 comments:
Post a Comment