WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) katika kipindi cha miezi 18, umepokea jumla ya Sh. bilioni 54.2 kutoka serikalini kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba za watumishi wa umma.
Mtendaji mkuu wa TBA, DAUDI KONDORO ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za wakala huo kwa waandishi wa habari ambapo amesema miradi hiyo ni pamoja na ule wa ujenzi wa nyumba 3,500 za watumishi wa umma katika eneo la Nzuguni jijini Dodoma .
“Serikali imeshatoa jumla ya Sh. bilioni 15.5 kwa kuanza utekelezaji wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa nyumba 150 ambao umefikia asilimia 81 na awamu ya pili ya ujenzi wa nyumba 150 za awamu ya pili ukiwa umefikia asilimia tatu”alisema Kondoro.
Ameeleza kuwa wamefanikiwa kuhuishwa kwa Sheria iliyoanzisha TBA. Mabadiliko ya Sheria hii itaiwezesha TBA kuongeza uwezo wa kuendeleza maeneo yake katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Pia itatoa nafasi ya kushirikiana na Sekta Binafsi jambo litakaloongeza fursa za uwekezaji na kuweza kujenga nyumba nyingi zaidi zitakazowanufaisha watumishi wa umma na wasio watumishi wa umma.
Aidha ameongeza kuwa wamefaanikiwa kutengeneza fursa za ajira na kutoa mafunzo kwa vitendo ambapo TBA imetengeneza ajira takribani 100,000 kwa vijana wenye ujuzi na wasio na ujuzi kupitia miradi inayotekelezwa nchini.
“Utekelezaji wa Miradi Mikubwa ya Kimkakati Kitaifa, TBA tumefanya ubunifu na kujenga nyumba 644 za Makazi kwa waliokuwa wakazi wa Magomeni Kota, nyumba za makazi kwa wataalamu katika mradi wa Bwawa la kufua umeme wa Mwalimu Nyerere katika Bonde la Mto Rufiji, usimamizi katika miradi ya ujenzi wa vihenge vya kisasa na Usimamizi wa ujenzi wa rada za kuongozea ndege”, ameeleza Kondoro
Aidha amesema wameendelea kusimamia na kukarabati
majengo ya Serikali ambapo mpaka sasa jumla ya nyumba na majengo 3,437
yameshakarabatiwa.
Vile vile wamefanya Udhibiti na Usimamizi Mzuri wa Rasilimali Fedha ambapo TBA inatumia mifumo iliyoandaliwa na Serikali katika kudhibiti mianya ya rushwa na kusaidia kufanya malipo kwa wakati na kwa ufanisi. Mifumo hiyo inajumuisha Mifumo ya Ulipaji Serikalini (MUSE), GePG, GRMS na manunuzi (TaNeps).
Hata hivyo amesema utumiaji wa mitambo na teknolojia ya kisasa ambapo TBA inamiliki mitambo ya kisasa inayosaidia utekelezaji wa miradi kwa ubora zaidi na kupunguza gharama za ujenzi.
0 comments:
Post a Comment