METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, February 15, 2023

RAS SINGIDA ATOA WIKI MOJA KUWEKA VYUMBA VYA MADARASA SAKAFU

 










KATIBU  Tawala Mkoa wa Singida Mwl. Dorothy Mwaluko   ametoa muda wa siku saba (wiki moja) kwa Afisa Elimu Kata, Mtendaji na kamati za shule kuhakikisha vyumba vyote vya madarasa katika Shule ya Msingi Kilimatinde iliyopo kata ya Kilimatinde Wilaya ya Manyoni vinawekwa sakafu.

Maelekezo hayo ameyatoa jana baada ya uwekaji wa jiwe la msingi katika jengo la ofisi ya Afisa Tarafa wa Tarafa husika ambapo pamoja na mambo mengine alitaka kupata taarifa ya shule hiyo ya msingi ikiwemo uwepo wa vyoo, madarasa na madawati.

Mwaluko alisema kwamba ni Mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba kila shule inapata ruzuku ya elimu bure (Capitation grant) ambapo alifafanua kwamba Mwalimu Mkuu pamoja na Afisa elimu wangeweza kuilekeza katika ujenzi wa sakafu hizo na kuwaondolea wanafunzi changamoto ya kusoma kwenye madarasa yenye vumbi.

"Mnapopata capitation msikimbilie kununua chaki angalieni namna itakavyowezekana ndani ya siku saba vyumba hivyo viwe vimewekewa sakafu, Afisa Elimu na Mtendaji shirikianeni muwashawishi wazazi na mafundi wajitolee nguvu kazi hiyo ikamilike" alisema Mwaluko.

Hata hivyo Afisa Elimu wa Kata hiyo Laura Athanas, alieleza kwamba katika shule hiyo wana jumla ya wanafunzi Mia nne (400) hivyo kupata ruzuku ndogo ikilinganishwa na shule nyinge jambo ambalo RAS alikataa vikali kwa mifano kwamba zipo shule zinapata fedha kidogo lakini bado wanaweza kufanya na kusimamia mipango ikakaa vizuri.

Aidha, RAS huyo alianzisha harambee ya kuchangia mifuko ya saruji ambapo alitoa mifuko mitano, Afisa Elimu naye akatoa mifuko miwili, huku Menejimenti ya Mkoa huo ilitoa jumla ya mifuko 10 kwa ajili ya uwekaji wa sakafu katika vyumba hivyo.

Katika hatua nyingine Mwaluko alitumia ziara hiyo kuwataka Watendaji na Maafisa Elimu Kata ya Nkonko kuwa wabunifu na kuimarisha usimamizi katika miradi ya Serikali inayotekelezwa katika maeneo yao ili kuharakisha maendeleo kwa wananchi.

RAS huyo alieleza kuwa  watendaji wanayo nafasi ya kuhimiza wananchi kujitolea nguvu kazi katika kusaidia shughuli za maendeleo ikiwemo ufatuaji wa tofali kwa ajili ya Ujenzi wa vyoo vya shule na usombaji wa mchanga na vifusi.

Mwaluko amewahimiza Maafisa Elimu kuhakikisha wanasimamia mashule pamoja na miundombinu yake ikiwemo ujenzi wa vyoo kwa maeneo ambayo yanachangamoto ili wanafunzi wapate utulivu.

Akitolea mfano wa shule ya Msingi Chikola ambayo ilikuwa haina vyoo alisema siku chache zilizopita alitembelea shule hiyo ambapo alimtaka Mkuu wa shule, Afisa Elimu Kata pamoja na Mtendaji kuhakikisha shule inakuwa na vyoo katika kipindi cha wiki mbili tofauti na hivyo

Ziara hiyo ilihusisha Menejiment ya Mkoa huo na walitembelea Ujenzi wa nyumba ya Afisa Tarafa kata ya Nkonko na Kilimatinde pamoja na ukaguzi wa Ujenzi wa shule ya msingi Solya na Hospitali ya Wilaya ya Manyoni.

 

 

 

 

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com