METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, November 20, 2021

WATUMISHI WA AFYA KITUNDA WALALAMIKIWA KUUZA DAMU

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora Rashid Magope (wa pili kulia) akiongea katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo.

Na Lucas Raphael,Tabora  

MADIWANI wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora wamesikishwa na tabia ya baadhi ya Wahudumu wa Kituo cha Afya Kitunda kilichoko wilayani humo baada ya kulalamikiwa na wananchi kuwa wanawauzia damu wagonjwa.

Wakiongea katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kilichofanyika jana walieleza kusikitishwa na Watumishi hao ambao hawajali maisha ya jamii kiasi cha kudiriki kuwauzia damu wagonjwa wenye uhitaji.

Mwalimu Peter Nzalalila, diwani wa kata ya Sikonge, akiongea kwa uchungu, alisema kuwa haingii akilini mgonjwa ambaye hajiwezi akija hospitalini hapo akiwa na upungufu wa damu anaambiwa alete hela kwanza ili aongezewe.

Alisisitiza kuwa jamii imekuwa ikihamasishwa kuchangia damu kwa lengo la kuwasaidia wale wote watakaokuwa na uhitaji wa huduma hiyo wakiwemo akinamama wajawazito, wagonjwa na wanaopata ajali.

‘Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi wa namna hii hatuwezi kuwafumbia macho,  tunaomba uchunguzi ufanyike na ikibainika kuwa malalamiko hayo yana ukweli watumishi hao wachukuliwe hatua kali za kinidhamu’, alisema. 

Aidha Nzalalila alisikitishwa na kitendo cha wananchi wenye Kadi za Bima ya Afya iliyoboreshwa (CHF) wanapoenda hospitalini kupata matibabu wanaambiwa dawa hamna hivyo wakanunue, alihoji huduma hiyo imeboreshwa kitu gani.

Diwani Yusuf Ahmed wa kata ya Kisanga alisema kuwa serikali ya awamu ya 6 ina dhamira njema ya kuboresha huduma za afya, elimu na nyinginezo lakini akasikitishwa na baadhi wa watumishi wasiozingatia maadili ya kazi zao.

Aliomba Ofisi ya Mkurugenzi kutofumbia macho malalamiko ya wananchi bali hatua stahiki zichukuliwe mara moja kwa wahusika pale inapobainika ukweli, vinginevyo wananchi wataendelea kuumia.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Rashid Magope ambaye ni diwani wa kata ya Tutuo, alisema huduma ya damu salama inatolewa bure hospitalini na kuongeza kuwa kama kuna watu wanawauzia wagonjwa hilo ni kinyume na taratibu.

Alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Seleman Pandawe kuchunguza malalamiko hayo na ikibainika yana ukweli wahusika wachukuliwe hatua za kinidhamu.

Aidha alisema huduma ya Bima ya Afya iliyoboreshwa inasuasua, waliojiunga hawapati huduma ipasavyo, jambo linalokwamisha watu wengine kujiunga, aliagiza lifanyiwe kazi ili lisikwamishe malengo ya serikali.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Seleman Pandawe alikiri kupokea malalamiko hayo na kuahidi kuwa ataunda Kamati ndogo ya kufuatilia tuhuma hizo, ikibainika zina ukweli atachukua hatua.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com