METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, February 13, 2023

MBUNGE CHEREHANI ATAKA WAKANDARASI UJENZI WA BARABARA KUSIMAMIWA IPASAVYO

Na Mathias Canal, Shinyanga

Mbunge wa Jimbo la Ushetu Mkoani Shinyanga Mhe Dkt Emmanuel Cherehani ameitaka serikali kuwasimamia na kuwafuatilia kwa ukaribu wakandarasi waliopata tenda ya ujenzi wa barabara.

Cherehani ametoa rai hiyo leo tarehe 13 Februari 2023 wakati akizungumza kwenye kikao cha bodi ya barabara ya mkoa wa Shinyanga.

Mbunge Cherehani amesema kuwa serikali ina wajibu wa kuwasimamia kwa karibu wakandarasi ili watekeleze majukumu yao ipasavyo kwani wamekuwa wakichelewesha ukamilishwaji wa miradi ya barabara jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo.

Amesema katika jimbo la Ushetu ni vyema barabara zote muhimu ziwekwe kwenye mpango wa ujenzi ili kurahisisha usafiri wa abiria na usafirishaji wa bidhaa mbalimbali ikiwemo za mazao na mifugo.

"Kwenye mtandao wa barabara za TANROADS jimbo la Ushetu lipo nyuma sana, Ukiangalia ukubwa wake unaweza kuunganisha Halmashauri ya Mji wa Kahama na Halmashauri ya Msalala lakini bado usilifikie hivyo ni muhimu kulitazama kwa karibu" Amesisitiza Dkt Cherehani

Amesema kuwa kuna ulazima wa jimbo la Ushetu kupewa kupaumbele kwenye mtandao wa barabara huku akitaka mikataba ya Ujenzi wa barabara inaposainiwa wabunge wapatiwe nakala ili kuifuatilia ipasavyo na kusimamia ubora wa barabara.

Kikao hicho pia kimejadiliana kuhusu taarifa za Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Shinyanga na taarifa ya Wakala wa barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) Mkoa wa Shinyanga.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com