Na Mathias Canal, Ushetu-Kahama
Mamia ya wananchi wa Jimbo la Ushetu katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga wamejitokeza kumlaki mbunge wa Jimbo hilo Mhe Dkt Emmanuel Cherehani wakati wa sherehe za kufikisha mwaka mmoja tangu awe mbunge wa jimbo hilo.
Akizungumza na wananchi hao leo tarehe 25 Februari 2023 wakati alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2022-2025 kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Februari 2023 Mbunge Cherehanu amewahakikishia wananchi hao kuwa serikali imedhamiria kutekeleza ilani ya CCM kwa vitendo.
Katika sherehe hizo zilizofanyika katika Kijiji cha Iramba Kata Igwamanoni mbunge huyo Mhe Emmanuel cherehani amesema kuwa kwa kipindi cha mwaka 2021/2022 Halmashauri ya Ushetu imeweza kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi 516,620,000.
Amesema mikopo hiyo imetolewa kwa vijana katika vikundi 14 yenye thamani ya Shilingi 123,800,000, kwa wanawake imetolewa shilingi 379,720,000 katika vikundi 41 huku kwa upande wa watu wenye ulemavu imetolewa shilingi 13,100,000 katika vikundi vitano.
Kuhusu sekta ya maji Mhe Cherehani amesema miradi ya maji iliyotekelezwa na kukamilika kwa kipindi cha mwaka wa fedha wa 2021/2022 kwa gharama ya shilingi 3,368,325,037.01 ni pamoja na mradi wa maji wa vijiji vya (Mpunze, Sabasabini na Iponyanholo), Vijiji vya (Igunda na Mhulidede), na kijiji cha Nyankende pamoja na kijiji cha Kisuke.
Amesema pia upanuzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Nyamilangano kwenda kijiji cha Mitonga na Ididi, na Upanuzi wa mradi wa maji wa Chambo kwenda kijiji cha Itumbili.
Mingine ni mradi wa ujenzi wa visima vifupi katika vijiji 11 vya Kipangu (2), Misayu (1), Salawe (1), Mwadui (1), Mulungu (1), Bukale (2), Ilemve (2), na Nussa (1) pamoja na ukarabati visima vifupi 15 katika vijiji vya Uyogo (2), Busenda (2), Nshimba (1), Makongolo (2), Bulima (1), Bugomba (1), Mbika (1), na Kabanga (1).
Kwenye sekta ya elimu Mbunge Cherehani amesema kuwa kupitia serikali kuu na wadau Halmashauri imeweza kujenga vyumba 104 vya madarasa ya sekondari kwa gharama ya shilingi 2,080,000,000.00 ikiwa ni pamoja na kujenga shule mpya ya sekondari iliyopo kijiji cha Mwadui.
Katika sekta ya kilimo Halmashauri ya Ushetu imepokea mbolea ya ruzuku kwa ajili ya zao la tumbaku Tani 15,000 sawa na shilingi 21,000,000.00, NPK Tani 18,000 sawa na shilingi 55,000,000,000.00
Kwenye zao la Pamba wakulima wamegawiwa mbegu za zao hilo zenye thamani ya shilingi Bilioni 6.2 hali itakayopelekea kuongeza wastani wa uzalishaji wa zao hilo kutoka milioni 8vilivyokuwa mwaka 2021/2022 hadi Tani milioni 18 kwa mwaka 2022/2023.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment