METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, September 23, 2016

LAPF NA TAASISI MBALIMBALI ZACHANGIA MIL.172 MAAFA KAGERA

top1
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hundi ya Shilingi milioni 16 kutoka kwa Dkt.  Ave Maria Semakafu (kulia), Berious Nyasebwa (wapili kushoto) na Benjamin Thomson wote  kutoka Group la Whats App la Leaders Forum ukiwa ni mchango wa group hilo kwa waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera. Makabidhiano hayo yalifanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dar es salaam Septemba 21, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
top2
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwashukuru viongozi wa Jumuiya ya Ahmadiyya ambao walitoa mchango wa shilingi milioni 10 kwa waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera, Septemba 22, 2016. Makabidhiano hayo yalifanyika ofisini kwa Waziri Mkuu jijini .Kutoka kushoto ni Sheikh Tahir Mahmood Chaundhry, Issa Mwakitalima, Khuram Shahzad na Jamil Mwanga.  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
top3
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea mchango wa tani  40 za saruji zenye thamani ya shilingi milioni 16.5 kutoka  kwa Dhruv Jog na Lebulu Victor (kulia) wote wa Kampuni ya ujenzi a  Advent ukiwa ni mchango kwa waahirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera Septemba  22, 2016. Makabidhiano hayo yalifanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dar es salaam. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

top4
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hundi ya shilingi milioni 100 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya VODACOM TANZANIA, Bw. Ian Ferrao (kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, Rosalynn Mworia ukiwa ni mchango kwa waarhirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera, Ofisini kwake  jijini Dar es salaam Septemba 22, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
top5
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hundi ya shilingi milioni 20 kutoka kwa Meneja wa Kanda wa LAPF, Amina Kassim (kulia) na  Kafiti Kafiti wa LAPF  ukiwa ni mchango wa Mfuko huo  kwa waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera. Makabidhiano hayo  yalifanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dar es salaam Septemba 22, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
top6
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea sehemu ya  msaada ya vyakula wenye thamani ya shilingi milioni 10 kutoka kwa viongozi wa Mfuko wa Kimataifa wa Art of Living ukiwa ni msaada kwa waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera, Septemba 22, 2016.  Kutoka kushoto ni Nishitha Kulshreshtha,  Nishit  Patel,  Neha Movaliya,Sharik Choughule ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa Shina la Pamba Road, Upanga  na Neha Movaliaya. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

TAASISI sita zikiwemo za dini na kijamii zimechanga jumla ya sh. milioni 172.5 zikiwa ni misaada kwa wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera Septemba 10, mwaka huu.

Mchango huo umepokelea leo jioni (Alhamisi, Septemba 22, 2016) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.

Akikabidhi hundi kwa Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, Bw. Ian Ferrao alisema kiasi cha sh. Milioni 100 kimekusanywa kutoka kwenye mfuko wa Vodacom Foundation pamoja na wadau wao.

Bw. Ferrao amesema kampuni ya Vodacom imekuwa mstari wa mbele kusaidiana na Serikali katika uboreshaji wa miradi mbalimbali za kijamii.

Taasisi nyingine iliyochangia ni Mfuko wa Pensheni wa LAPF  ambapo Meneja wa Kaya ya Dar es Salaam, Amina Kassim amemkabidhi Waziri Mkuu hundi ya sh. milioni 20.

Pia Jumuiya ya Kiislam Ahmadiyya imekabidhi msaada wa sh. milioni 10 kati ya hizo sh. milioni nne ni fedha taslimu na zilizobaki ni mabati na mifuko ya saruji.

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya Advent, Dhruv Jog amemkabidhi Waziri Mkuu msaada wa tani 40 za saruji yenye thamani ya sh. milioni 16.5 na kusema  kwamba wameshtushwa na tukio hilo na tayari saruji hiyo imeanza kupelekwa Kagera.

Kwa upande wake mwakilishi wa Taasisi ya kimataifa ya Art of Living, Neetu Kulshreshtha wametoa msaada wa vyakula mbalimbali pamoja dawa vikiwa na thamani ya sh. milioni 10.

Dk. Ave Maria Semakafu amemkabidhi Waziri Mkuu hundi ya sh milioni 16 kwa niaba ya makundi mawili ya mtandao wa kijamii wa WhatsApp. Makundi hayo yanaitwa Leaders na Uongozi.

Akitoa shukrani kwa waliotoa michango yote hiyo, Waziri Mkuu amewashukuru kwa misaada hiyo na kuahidi kuwa Serikali itahakikisha michango hiyo inafikishwa Kagera kwa walengwa.

“Tunashukuru sana kwa michango yote. Tunashukuru na makundi ya WhatsApp ya Leaders na Uongozi ambayo nayo yameamua kuja kutuchangia. Michango hii inaonyesha kuguswa na mapenzi ya dhati kwa waliopatwa na maafa,” amesema. 

Waziri Mkuu amesema Serikali inakamilisha tathmini ya maafa hayo na kuahidi kutoa taarifa ya kiasi kilichokusanywa na kiasi kilichotumika. Amewaomba wananchi waliotoa ahadi zao za michango wakamilishe ahadi zao.

Akaunti ya maafa imefunguliwa katika Benki ya CRDB yenye Namba. 015 222 561 7300 kwa jina la KAMATI MAAFA KAGERA – Swiftcode: CORUtztz na namba za simu za mkononi zinazotumika kupokea michango hiyo ni 0768-196-669 (M-Pesa), au 0682-950-009 (Airtel Money) au 0718-069-616(Tigo Pesa).

Tetemeko hilo lililotokea Jumamosi, Septemba 10, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 17 na wengine 440 walijeruhiwa kati yao watu 253 walifikishwa Hospitali ya Mkoa, 153 walilazwa, 113 walitibiwa na kuruhusiwa na wengine 38 wanaendelea na matibabu ambapo kati yao watu 23 wamefanyiwa upasuaji mkubwa na wanaendelea vizuri. 

Pia tetemeko hilo limesababisha nyumba 2,063 kuanguka huku nyingine 14,081 zikiwa katika hali hatarishi baada ya kupata nyufa na 9,471 zimepata uharibifu mdogo huku wananchi 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com