METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, February 7, 2023

IKUNGI YATOA SHILINGI MILIONI 141 MIKOPO KWA VIKUNDI 12 VYA AKINA MAMA, VIJANA NA WENYE UHITAJI

 

Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi wakiwa kwenye picha ya pamoja na wanufaika wa mkopo wa Milioni 141 uliotolewa na Halmashauri hiyo kwa vikundi vya akina Mama,Vijana na Wenye Mahitaji Maalum leo February 7 2023 baada kupokea hundi kwenye ofisi za Halmashauri. 

Mkurugenzi wa halmashauri ya Ikungi Justice Kijazi  pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Ally Mwanga wakimkabidhi Mnufaika Cherehani.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ikungi Ally Mwanga, Mkurugenzi wa Halmashauri Justice Kijazi wakikabidhi hundi ya Fedha za Mkopo kwa wanufaika wa Ikungi.


Makabidhiano yakiendelea 


Picha ya Pamoja ya Wanufaika wa mkopo wa Milioni 141 na vyerehani vitatu  kutoka Halmashauri ya Ikungi.


Na Hamis Hussein - Ikungi, Singida

HALMASHAURI ya Wilaya ya Ikungi kupitia kamati ya Huduma za jamii imekabidhi hundi yenye thamani ya shilingi Milioni 141 na vyerehani vitatu kwa vikundi 12 vya akina mama,Vijana na watu kwenye mahitaji maalum ikiwa ni utekelezaji wa sheria ya utoaji mikopo ya asilimia 10 ya makusanyo ya mapato ya ndani.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya mikopo hiyo ambayo imetolewa kwenye nusu ya kwanza ya bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ally Juma Mwanga amesema mikopo hiyo itawapa fursa akina mama na vijana kuongeza vipato vyao na kuchochea maendeleo.

Mwanga alisema halmashauri hiyo kutenga asilimia 10 ya makusanyo ya Mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo hiyo itaviiunua vikundi ambavyo vilishindwa kufanya shughuli za maelekezo kwa kukosa mitaji.

"Halmashauri imekuwa ikitenga fedha hizi ambazo ni mapato ya makusanyo ya ndani na hizi fedha tunazowapatia  zitachochea maendeleo kwa akina Mama na wenye mahitaji maalum kwa sababu wengi walikuwa wanakosa mitaji ya kufanya  kazi za maendeleo kama vile ujasiriamali” Alisema Mwanga.

Makamu mwenyekiti kamati hiyo ambaye ni diwani wa kata ya Isuna Stephano Misai aliwaasa wanufaika hao kutumia fedha hizo katika kuyafikia malengo yaliyo kusudiwa na kuhakikisha kwamba mikopo hiyo ambayo haina riba inarejeshwa kwa wakati ili na wengine wapate fursa hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Ikungi Justice Kijazi akiwa kwenye hafla hiyo alisema halmashauri hiyo inatekeleza sheria ya kutenga na kutoa mikopo hiyo ya asilimia kumi kwa vikundi vya akina mama,Vijana na wenye uhitaji maalum.

"Tumeendelea kutekeleza sheria ya kutenga na kutoa mikopo kwa vikundi vilivyoanishwa,katika mwaka wa fedha 2022/2023  tumefanikiwa kutoa milioni 141 fedha za mikopo pamoja na vyerehani 3 kwa vikundi kumi na mbili vya wanufaika". alisema Kijazi.

Alivitaja vikundi vilivyonufaika na mikopo hiyo ya halmashauri ambayo vimegawanyika sehemu tatu ambazo ni makundi ya akina Mama ambayo ni kikundi Cha ushirika-siuyu,Kikundi Cha Jonelaa -Siuyu,Kikundi Cha Heshima wanawake -Ikungi, Tumaini Stara-Iyumbu, Mshikamano-Iyumbu, Faraja- Mgungira, Igembensabo-Ng'ongosoro, Ipililo-Ng'ongosoro.

Kwa upande wa vikundi vya Vijana ni pamoja na Kidundu-Kipunda, Roho safi-Iyumbu, Be the Light-Kipumbuiko, Vijana Chapakazi -Ikungi huku upande wa kundi la kwenye ulemavu likiwa ni Kwajaa kilichopo Matongo Ikungi.

Ikumbukwe kuwa katika miaka mitano iliyopita halmashauri hiyo imefanikiwa kutoa shilingi milioni 600 fedha za mikopo kwa wanufaika.

 

 

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com