Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda ameitaka Bodi ya tume ya Elimu ya vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kutokubali kutumika badala yake wafanye kazi kwa kuzingatia Sheria na kutenda haki katika kutekeleza majukumu yao.
Prof.Mkenda ameyasema hayo leo Januari 19,2023 Jijini Dodoma wakati akizindua bodi hiyo na kusema kuwa ina kazi kubwa ya kuwezesha na kudhibiti hivyo watumie nafasi hiyo kuifungua nchi katika sekta ya Elimu.
"Msiangalie mtu usoni nyinyi chapeni kazi kikubwa ni kuzingatia Sheria na kufanya kwa haki kwani bodi yenu ina kazi kubwa mbili ya kwanza kuwezesha na pili ni kudhibiti, sasa kazi ya kudhibiti ina lawama sana na lazima mkubaliane nazo,"
"Kazi yenu ina lawama sana hasa pale mnapotaka kutekeleza jukumu la kudhibiti hapo lazima mguse watu hivyo msiogope kwani kufanya hivyo itasaidia kuongeza ubora katika sekta yetu ya Elimu hasa Elimu ya vyuo vikuu ambayo ndio muhimili wa Taifa letu," Amesisitiza Mkenda
Waziri Mkenda pia ameitaka Bodi hiyo ya TCU kuhakikisha wanawezesha vyuo kufanya udahili na kuhakikisha elimu inayotolewa Vyuoni iwe bora na Ufaulu uwe mzuri ili kutengeneza taifa lenye watu wasomi wanaokidhi vigezo.
Pia Prof.Mkenda ameitaka Bodi hiyo kuwezesha utambuzi wa vyuo vikuu vya nje ya nchi ikiwezekana kwenda kufanya uchunguzi kuhusu ubora na nafasi ya vyuo hivyo katika nchi zao ili kuwasaidia vijana wa kitanzania wanapokwenda kusoma nje wasome katika vyuo bora na vyenye ushindani.
"Jaribuni kutambua vyuo vinavyofundisha wanafunzi wetu huko nje na mjaribu pia kufanya tafsiri ya elimu inayotolewa katika vyuo hivyo ili kuwawezesha wanafunzi wetu wanaomaliza huko nje na kurudi nyumbani waajirike tusiishie tu kuwapeleka alafu kwenye soko la ajira hatuwaoni,"amesema Prof.Mkenda
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume hiyo Prof.Penina Mlama amemhakikishia Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe.Prof Adolf Mkenda kuwa watatekeleza maelekezo yote aliyowaagiza iliwemo kuifungua nchi kimataifa kwa kuwapeleka wanafunzi wengi kusoma Vyuo vya nje ya nchi,Kuongezeka kwa kasi ya Udahil,kusimamia ubora wa elimu inayotolewa na kuhakikisha vyuo vikuu vinasimama imara kuhimili na kuyamudu mabadiliko yanayotokea duniani.
Credit, Okuly Blog
0 comments:
Post a Comment