Na Dotto Mwaibale, Manyoni
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limetoa mifuko 75 ya saruji yenye thamani ya Sh. Milioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa hosteli ya wasichana katika Sekondari ya Kintinku iliyopo wilayani Manyoni mkoani Singida.
Akizungumza wakati akikabidhi saruji hiyo kwa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Fadhili Chimsala kwa niaba ya mkurugenzi mkuu wa Shirika hilo, Meneja wa NHC Mkoa wa Singida, Judith Mwalongo alisema saruji hiyo ina kwenda kusaidia kukamilisha ujenzi wa hosteli hiyo na kuondoa adha ya kutembea umbali mrefu kwa wanafunzi wa shule hiyo wakati wa kwenda shuleni.
"Wanafunzi wa shule hii wanatembea umbali wa zaidi ya kilomita 10 kila siku wakati kwenda na kurudi nyumbani hali inayowafanya washindwe kupata masomo yao vizuri na sisi baada ya kuiona changamoto hiyo tukaamua kuchangia ujenzi wa hosteli hii" alisema Mwalongo.
Mwalongo alisema shirika hilo lina utaratibu wa kushiriki shughuli za kijamii kwa kusaidia katika mambo ya maendeleo kama walivyofanya katika shule hiyo.
"Shirika letu lina utaratibu wa kurudisha faida tunayoipata kwa jamii kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo (Cooperate Social Responsibility) na leo tumekuja hapa Manyoni kushiriki ujenzi wa Hosteli katika Shule ya Sekondari ya Kintinku kwa mara nyingine tena kwani tulishawahi kutoa msaada kama huu na yote hii ni kuunga mkono jitihada za Serikali za kusaidia shughuli za maendeleo" alisema Mwalongo.
Mwalongo alitoa ahadi ya kuendelea kusaidia ujenzi huo pindi watakapopata nafasi ya kufanya hivyo lengo likiwa ni kuhakikisha ujenzi wa hosteli hiyo unakamilika na wanafunzi wanaitumia.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Fadhili Chimsala akipokea msaada huo alilishukuru shirika hilo kwa msaada ambao wamekuwa wakiutoa mara kwa mara katika halmashauri hiyo na kuwa wamekuwa wadau wao wakubwa wa maendeleo.
"Kweli NHC mnafanya kazi kubwa katika halmashauri yetu hatuna maneno mengi zaidi ya kuwashukuru tunaomba hizi salamu zetu mtufikishie kwa mkurugenzi wenu mkuu Nehemia Mchechu na msichoke kutusaidia" alisema Chimsala.
0 comments:
Post a Comment