NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja ameiambia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii itayafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na kamati hiyo kuhusu kuzifanyia upya uhakiki hoteli na loji za kitalii ambazo hazifanyi kazi vizuri ili kukabiliana na changamoto ya huduma za malazi kwa watalii hapa nchini.
Mhe. Mary
Masanja ameyasema hayo kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii leo jijini
Dodoma mara baada ya kupokea maoni, ushauri na maelekezo yaliyotolewa na Kamati
ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii
kuhusu taarifa ya Wizara ya Utendaji kazi wa Hoteli na Loji za kitalii
za Serikali zilizobinafsishwa.
Amesema Tanzania
imekua ikipokea watalii wengi hali iliyosababisha kuongezeka kwa mahitaji ya
huduma za malazi kwa watalii kufuatia kazi kubwa iliyofanywa na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutangaza vivutio vya
utalii kupitia Filamu ya Royal Tour.
“Namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuzindua filamu ya Royal Tour
ambayo kwa sasa matunda yake yanaonekana kwa kuongezeka kwa mahitaji ya huduma
za malazi kwa watalii hapa nchini”
amebainisha Mhe. Masanja.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe.
Ally Juma Makoa ameeleza kuwa Wizara ya
Maliasili na Utalii inapaswa kufanya maamuzi kwa kufuata sheria zilizopo ili
hoteli na loji ambazo hazifanyi kazi ziweze kutoa huduma ili kwenda na kasi ya
idadi ya watalii pia kuongeza mapato yatokanayo na biashara za utalii, kuongeza
tija na ufanisi katika uendeshaji wa hoteli za kitalii.
“Inabidi tufanye maamuzi ya haraka sana
ya kuona namna gani tunaweza kuboresha huduma za hoteli na loji ambazo
hazifanyi kazi ili kuendana na kasi ya idadi ya watalii wanaokuja nchini baada
ya kuzinduliwa kwa Royal Tour”
amesisitiza Mhe. Makoa.
Awali
akiwasilisha taarifa ya hali ya loji na hoteli za kitalii Afisa Usimamizi wa
Fedha Mkuu kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina Thabiti Dokodoko amesema uwekezaji
katika hoteli na loji umeisaidia Serikali kuingiza kiasi cha shilingi bilioni
60.38 kwa kipindi cha miaka mitano (2018/19-Desemba, 2022).
Ameongeza kuwa
uwekezaji katika hoteli na loji za kitalii unalenga katika kutatua changamoto
ya huduma za malazi hususan idadi ya vyumba na vitanda.
0 comments:
Post a Comment