METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, January 25, 2023

MKOA WA RUVUMA ULIVYODHAMIRIA KUPUNGUZA UDUMAVU NA UTAPIAMLO


KATIBU Tawala Mkoa wa Ruvuma Ndugu Stephen Ndaki ameongoza kikao cha Kamati ya Lishe Mkoa ambacho kimelenga kupokea majukumu na viashiria vya kupima utendaji kazi wa Kamati ili kupunguza udumavu na utapiamlo.

kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mipango Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma pia kimepokea taarifa ya utekelezaji wa mkataba wa Lishe kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2022.

Akizungumza kwenye kikao hicho Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma amelitaja chimbuko la mkataba wa lishe unaotekelezwa katika ngazi zote,kuwa umetokana na utafiti ambao ulifanyika mwaka 2017 ambao ulibaini mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ukiwemo Mkoa wa Ruvuma iliyoongoza kwa udumavu.

“Tulikuwa tunajiuliza mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ndiyo inaongoza kwa uzalishaji wa vyakula vya aina zote sasa tukawa tunajiuliza chakula ni kingi tumedumaa vipi’’,alisema Ndaki.

Amesema wakati utafiti huo umefanyika Mkoa wa Ruvuma kwenye udumavu ulikuwa na asilimia 42 ya udumavu hivyo kuwa juu ya udumavu wa kitaifa ambao ni asilimia 39.

Hata hivyo amesema Mkoa umekuwa unachukua hatua mbalimbali za kupunguza kiwango cha udumavu ambapo umefanikiwa kupunguza kiwango cha udumavu kwa asilimia moja kutoka asilimia 42 hadi 41 kiwango ambacho amesema bado kipo juu.

Amesisitiza kuwa udumavu unapowakumba Watoto chini ya miaka mitano unaathiri hadi ukuaji wa ubongo hivyo ametoa rai kwa wajumbe wa Kamati ya Lishe Mkoa wa Ruvuma kila mmoja kuwajibika kwenye eneo lake ili kutoa elimu endelevu itakayosaidia kupunguza udumavu na utapiamlo katika Mkoa na Taifa kwa ujumla.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dr.Luois Chomboko  akizungumza kwenye kikao hicho amesema ili kukabiliana na changamoto ya udumavu tangu mwaka 2017,serikali iliamua kutoa mkataba wa utekelezaji wa afua za lishe.

Amesisitiza kuwa mikataba hiyo imekuwa inatekelezwa  na kwamba Septemba 30,2022,mkataba wa lishe awamu ya pili umesainiwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambao unatekelezwa katika ngazi za mikoa na Halmashauri.

“Lishe ni msingi wa uchumi na maendeleo na afya ya binadamu,tupo katika utekelezaji wa Mpango Mkakati Jumuishi wa pili wa Taifa wa Lishe unaoanzia mwaka 2021 hadi 2026’’,alisema Dr.Chomboko.

Hata hivyo amesema serikali imeahidi kuchangia asilimia 10.5 ya utekelezaji wa mpango huo ambao ni sawa na shilingi bilioni 67.22 katika utekelezaji na kwamba fedha hizo zitakuwa zinatoka katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa na Mkoa.

Kwa upande wake  Mratibu wa Lishe Mkoa wa Ruvuma Neema Mtekwa amesema katika kukabiliana na utapiamlo na udumavu,Mkoa umetoa maelekezo kwa wakurugenzi ili elimu ya lishe iendelee kutolewa kwa jamii na Taasisi.

Mtekwa amesema shule zote zimeelekezwa kutumia unga ulioongezwa virutubisho,kulima mahindi na maharage lishe ili kuongeza upatikanaji wake na kwamba kupitia kikao cha Mkoa wazabuni wameelekezwa kupeleka mahindi lishe shuleni. 

Kutokana na hali ya lishe na udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano kuwa mbaya nchini,Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,aliagiza kuwepo kwa mkataba wa usimamiaji wa shughuli za Lishe baina yake na Wakuu wa Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.

Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikali Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com