METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, January 19, 2021

JKT Yasitisha Mafunzo kwa Kundi la Kujitolea

Kaimu Mkuu wa Utawala  wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kanali Hassan Mabena akieleza kwa waandishi wa habari  kuhusu kusitishwa kwa mafunzo ya kundi la kujitolea kwa mwaka 2020/2021 wakati wa mkutano uliofanyika makao makuu ya Jeshi hilo wilayani Chamwino mkoani Dodoma leo Januari 19, 2021, Mafunzo hayo yalipangwa kuanza hivi karibuni katika makambi mbalimbali ya JKT.

Sehemu ya waandishi wa habari wakifuatilia mkutano wa Kaimu Mkuu wa Utawala  wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kanali Hassan Mabena  wakati akieleza  kuhusu kusitishwa kwa mafunzo ya kundi la kujitolea kwa mwaka 2020/2021 yaliyokuwa yaanze hivi karibuni katika makambi mbalimbali hapa nchini hadi yatakapotangazwa tena.

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limesitisha kwa muda Mafunzo kwa  kundi la kujitolea kwa mwaka 2020/2021 kwa vijana waliokuwa wamechaguliwa  kushiriki mafunzo hayo yaliyotarajiwa kuanza hivi karibuni nchini kote.

Hayo yamesemwa  leo  na Kaimu  Mkuu wa Utawala, Kanali Hassan Mabena wakati wa mkutano wake  na waandishi wa habari uliofanyika  Makao Makuu ya Jeshi hilo wilayani Chamwino mkoani Dodoma.

“Kutokana na kusitishwa kwa mafunzo hayo, JKT inawataka  vijana wote ambao walichaguliwa na kuripoti makambini kwa ajili ya kuhudhuria mafunzo ya JKT kwa kujitolea warejee majumbani kwao” alisisitiza Kanali Mabena.

Pamoja na hayo, Kanali Mabena amewataka vijana  ambao walikuwa hahawajaripoti wasiende kuripoti katika makambi waliyopangiwa mpaka watakapotangaziwa tena.

Jeshi la Kujenga Taifa limekuwa likiwajengea vijana uwezo wa kujiajiri kupitia stadi za maisha wanazopata katika mafunzo yanayotolewa  kwa mujibu wa sheria na yale ya vijana kujitolea, hivyo kuwawezesha kuwa wazalendo wanaoshiriki kikamilifu katika ujenzi waTaifa.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com