METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, January 21, 2021

WAZIRI KALEMANI APONGEZWA NA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI KWA KASI YA KUSAMBAZA UMEME VIJIJINI

Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani akiwasilisha Taarifa ya Wizara ya Nishati Kuhusu Muundo na Majukumu ya Wizara kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini leo tarehe 20 Januari, 2021 Bungeni jijini Dodoma. Kulia kwake ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Leonard Masanja. 

Makamu M/Kiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Seif Khamis Gulamali na Katibu wa kamati hiyo Bi. Felister Mgonja pamoja na wajumbe wa Kamati tajwa hapo juu, wakifuatilia kwa makini maelezo ya Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani alipokuwa akiwasilisha Taarifa ya Wizara ya Nishati Kuhusu Muundo na Majukumu ya Wizara kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini leo tarehe 20 Januari, 2021 Bungeni jijini Dodoma. Kulia kwa Waziri Kalemani, ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Leonard Masanja. 

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imempongeza Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani kwa kasi ya kusambaza umeme vijijini ambapo hadi sasa zaidi ya asilimia 80 ya vijiji vyote nchini vimepelekewa huduma ya umeme.

 

Pongezi hizo zimetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Seif Khamis Gulamali baada ya Taarifa ya Wizara ya Nishati kuhusu Muundo na Majukumu ya Wizara ya Nishati kuwasilishwa kwenye kikao cha Kamati hiyo tarehe 20 Januari, 2021, bungeni jijini Dodoma.

 

Mhe. Seif Khamis Gulamali amesema kuwa, kasi ya usambazaji umeme vijijini ni kubwa na yawezekana Tanzania ni nchi ya kwanza Afrika katika usambazaji wa umeme vijijini.

 

Akizungumza kufuatia pongezi hizo, Waziri Kalemani amesema, Wizara ya Nishati itahakikisha vijiji vyote 2200 vilivyobakia ambavyo bado havijaunganishwa na umeme, vitapatiwa huduma hiyo ndani ya miezi 18 kuanzia sasa.

 

Akijibu swali kuhusu maeneo yenye changamoto ya ukatikaji wa umeme hapa nchini, Waziri Kalemani ameeleza kuwa, kwa upande wa Dodoma , Dar-es-salaam na Mwanza, Wizara ya Nishati kupitia TANESCO imefunga mitambo yenye uwezo wa kutoa umeme wa kutosha hivyo endapo kutatokea kukatika kwa umeme,  kutakuwa kumetokana na hitilafu za kiufundi.

 

Aidha, Waziri Kalemani amekiri kuwa, kulikuwa na changamoto ya umeme kwa Mkoa wa Ruvuma isipokuwa eneo la Masasi na Tunduru na kueleza kuwa kuna vifaa vya kuboresha nguvu ya umeme ( Automatic Voltage Regulators - AVR ) vinaendelea kufungwa ili kuongeza umeme uwe mkubwa kwa ajili ya watumiaji.

Aliongeza kuwa, ufungaji wa vifaa vya AVR unafanyika pia katika Jimbo la Nyasa na utakuwa umekamilika ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa na hivyo upatikanaji wa umeme katika maeneo husika utaimarika.

 

Akijibu swali kuhusu ratiba ya utekelezaji wa kazi za Wakandarasi wa umeme katika maeneo yanayopitiwa na miradi ya umeme, Waziri Kalemani amesema, "tumewasihi sana Wakandarasi wanapofika kwenye maeneo husika, wakutane nanyi Waheshimiwa Wabunge na Wakuu wa Wilaya. Kwanza, kutoa taarifa kuwa wameingia kwenye maeneo yenu lakini pia wajue wanaanzia maeneo gani yenye kero ili kushauriana nao mahali pa kuanzia. Tutakapokuwa tunazindua tutawakabidhi kwenu Wakandarasi hao ili mkae nao wajue waanzie wapi." Amesema Dkt. Kalemani

 

Akielezea kuhusu upatikanaji wa mafuta kwa maeneo ya vijijini na miji midogo, Dkt. Kalemani ameieleza Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa, Wizara ya Nishati ina mpango wa kuendelea kusambaza vituo vya mafuta katika maeneo ya vijijini na miji midogo kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa nishati ya Mafuta na usalama kwa watumiaji wa maeneo tajwa.

 

Waziri Kalemani amefafanua kuwa, katika utekelezaji wa suala hilo, kanuni zinapitiwa ili kupunguza gharama za uwekezaji wa vituo vya mafuta katika maeneo ya vijijini na miji midogo ili kuweza kupata wawekezaji wengi kwenye maeneo hayo.

 

Ameongeza kuwa, Wizara ya Nishati, inafikiria kujenga vituo rahisi vya pampu moja, ambavyo uwekezaji wake utakuwa nafuu.

 

Vikao vya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini vilivyoanza jijini Dodoma tarehe 20 Januari, 2021, vinatarajiwa kukamilika tarehe 22 Januari, 2021.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com