MENEJIMENTI ya Chuo cha Misitu Olmotonyi kilichopo jijini Arusha imetakiwa kubuni mikakati mipya ya kujiongezea mapato ili kuongeza udahili wa wanafunzi, motisha kwa wafanyakazi pamoja na kuzalisha mazao yatokanayo na misitu zikiwemo fenicha zenye ubora
Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii, Mary Masanja ameyasema hayo jana katika kikao
kilichofanyika kwenye ukumbi wa chuo hicho Jijini Arusha ambapo amesema kuna haja
ya kukiboresha chuo hicho ili kiweze kuleta tija kwa Taifa.
“Moja ya kazi ya kufanya ni kuendelea
kubuni vyanzo vya mapato lakini pia ni lazima muwe na maandiko mahususi
yanayojenga hoja kuwafanya wanaotoa ukomo wa bajeti waweze kuliona kwa macho ya
kipekee” alisisitiza
Naibu Waziri Masanja.
Naibu Waziri
Masanja alisema kuna haja ya kufanya mabadiliko hasa katika mfumo wa uendeshaji
wa chuo hicho kwa kuwafundisha vijana vitendo zaidi kuliko nadharia ili
kuwawezesha kuchakata mazao ya misitu yenye ubora wa hali ya juu yatakayoweza kushindanishwa na bidhaa
zinazotoka nje ya nchi.
Aidha, Masanja
aliilekeza Menejimenti hiyo kuzalisha vijana wakomavu na wenye taaluma ili wasaidie katika uhifadhi
wa misitu kutokana na nchi kukumbwa na changamoto ya uvamizi wa misitu na ukataji wa miti hovyo.
Amesema Wizara
ya Maliasili na Utalii ina matumaini makubwa na vijana wanaopatiwa ujuzi katika
chuo hicho na kwamba wanakwemda kuwa
Mabalozi wa kuielimisha jamii kuhusu
umuhimu wa kutunza misitu sambamba na kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya
misitu
Katika hatua
nyingine, Mhe. Masanja amesema Wizara itaendelea kutatua changamoto zinazokikaboli
chuo hicho ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya watumishi na kuboresha muundo
wa watumishi.
Awali,
akiwasilisha taarifa ya utekelezaji Makamu Mkuu wa Chuo hicho , Stephen
Kingwele amesema chuo kinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa watumishi unaopelekea
kuajiri watumishi wa mkataba ili kusaidia nguvukazi.Pia ameishukuru Wizara ya
Maliasili na Utalii ambayo imekuwa ikisaidia fedha za utekelezaji wa majukumu
kupitia Mfuko wa Misitu.
Naye, Mkuu wa
Wilaya ya Arumeru Mhandisi Richard Ruyango amemshukuru Naibu Waziri kwa kufanya
ziara katika chuo hicho kwa kuwa ndio mwanzo wa kutatuliwa kwa changamoto
mbalimbali zinazokikabili.
Chuo cha Misitu
Olmotonyi kilianzishwa mwaka 1937 kwa lengo la kuzalisha wafanyakazi katika
sekta ya misitu ili kuwepo na uhifadhi endelevu.
0 comments:
Post a Comment