Na Mathias Canal, WEST-Kilimanjaro
Mapitio ya sera na mitaala yameshirikisha wadau mbalimbali na kwamba kwa sasa yapo tayari kwa mjadala wa kitaifa kuhusu mapendekezo ya sera ya elimu na mitaala.
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imefanya kazi kubwa katika mchakato mzima wa kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali ambapo kwa sasa mchakato wa ndani ya Wizara umekamilika unasubiri mchakato wa ndani ya serikali kabla ya kuandaa kongamano maalumu la kukusanya maoni ya wananchi.
Katika Mapitio hayo ya Sera na Mitaala serikali imezingatia ujenzi, mapitio na maboresho ya vyuo vyote vya ualimu kwani ndio mboni na jicho la elimu nchini.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 9 Januari 2023 wakati akizungumza na uongozi pamoja na wanafunzi wa Chuo cha Ualimu Marangu wakati akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Kilimanjaro.
Waziri Mkenda amesema kwa sasa kuna jumla ya Vyuo 35 vya serikali na vyuo vingine vya taasisi na vile vya binafsi hivyo kuna kila sababu ya kuvitazama kwa umakini mkubwa ili kuboresha elimu nchini.
Waziri Mkenda amesema kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itaimarisha Uboreshaji wa vyuo vya ualimu ikiwemo miundombinu na upatikanaji wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia ili kuimarisha sekta ya elimu nchini.
Pia Waziri Mkenda amesema kuwa Serikali itaweka mkakati mzuri wa elimu ili kusaidia walimu nchini kuweza kujiendeleza pamoja na kuongeza ujuzi.
Mara kadhaa Prof Mkenda amesikika akisisitiza kuwa ndoto ya Serikali ni kuona mwalimu anajiendeleza ili aweze kuwa mwalimu bora hivyo msimamo wa serikali ni kuwaruhusu walimu kujiendeleza ndani na nje ya nchi.
Akizungumza Tarehe 9 Octoba 2023 kwenye kilele cha siku ya Walimu katika Wilaya ya Bukombe Mkoani Geita Waziri Mkenda alisema kuwa “Mwalimu akiomba ruhusa ya kwenda kusoma mpe ruhusa, mwalimu ni ufunguo wa maisha katika maendeleo ya nchi yetu, mafunzo kazini yataendelea, Serikali ya awamu ya sita imetenga bajeti kwa ajili ya kuwaendeleza walimu,”
MWISHO
0 comments:
Post a Comment