OR-TAMISEMI
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Angellah Kairuki amekerwa na hali ya asilimia 55.2 ya wanafunzi waliotakiwa kujiunga na kidato cha kwanza mkoani Tanga kutoripoti shule.
Mhe. Kairuki ametoa kauli hiyo mkoani Tanga Tar 16.01.2023 wakati akizungumza na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule za Sekondari, Walimu Wakuu wa Shule za Msingi na viongozi wa Elimu ngazi ya Halmashauri kwenye kikao kazi cha Uboreshaji wa Usimamizi wa Elimumsingi na Sekondari katika shule ya sekondari Tanga ufundi.
Amesema takwimu za wanafunzi walioripoti kidato cha kwanza si ya kuridhisha katika mkoa huo.
“Ukiangalia kwenye elimu ya awali mpaka sasa uandikishwaji ni asilimia 82 , lakini nilitamani nisikie kwa upande wa wanafunzi wenye mahitaji maalum ni asilimia ngapi ili nao tusiwaache nyuma.”
“Kwa upande wa uwandikishwaji wanafunzi darasa la kwanza mmefikia asilimia 87.7 lakini changamoto inakuja kwenye kuripoti wanafunzi wa kidato cha kwanza.”
Amesema mpaka Januari 13, mwaka huu zaidi ya wanafunzi 27,867 ambao ni sawa na asilimia 55,2 hawajaripoti shule huku walioripoti kwa Wilaya ya Kilindi ni asilimia 11 pekee.
Mhe. Kairuki amesema mpaka sasa ni asilimia 44.8 pekee ya wanafunzi ndio wameripoti shule katika mkoa huo na kusisitiza kuwa ni lazima kila kiongozi kuhakikisha takwimu hizo zinabadilika ndani ya muda mfupi.
Amesema kati ya wanafunzi 27,867 ambao hawajaripoti shule, asilimia kubwa imechangiwa na Wilaya ya Kilindi ambayo ni asilimia 11 pekee ndio walioripoti huku Korogwe Mji ikiwa ni asilimia 22.78, Korogwe TC asilimia 30.21, Handeni TC asilimia 42.55, Handen DC asilimia 45.86, Bumbuli asilimia 53.26, Mkinga asilimia 27.98 Muhenza asilimia 50 Pangani 52 na Tanga jiji 76.23
“ Je hii ni sawa jamani? Hivyo kila mmoja kwa kadri inavyowezekana takwimu hizi zibadilike ndani ya muda mfupi sana. Haiwezekani tupo siku 16 ya mwezi wa kwanza na watoto zaidi ya 27,867 hawajaingia shule. “
“Kila mmoja arudi, ajitafakari kwa vitendo tufanye tathimini sahihi ya kufuatilia mtoto mmoja baada ya mwingine na bahati nzuri sana wengi wa wanafunzi wanatoka mkoa huu huu na wanatoka kwenye meneo yetu ambako tuna waratibu wa Elimu kata, Maafisa Elimu halmashauri, rudini katika orodha angalieni nani yuko wapi na kwa nini hajafika shuleni.”
Amesema takwimu zinaonesha kuwa Wilaya ya Lushoto ni ya mwisho katika uandikishaji wa elimu ya awali huku Pangani ikiwa na asilimia 48 na Korogwe DC ina asilimia 67 na kusisitiza haja ya kubadilika,
“Angalau tungekuwa bado mwezi mmoja kufungua shule lakini tayari watoto wamesharipoti siku saba sasa, na ukomo tuliojipangia tayari siku 16 zimepita je unatarajia ni nani ashuke afanye uhamasishaji wa uandikishaji kama sip nyie?”
Amesema kitendo cha watoto kutoandikishwa na kutoripoti kidato cha kwanza kunaondoa maana ya juhudi za Serikali za kujenga madarasa.
“ Haya madarasa tuliyoyajenga yatakuwa na maana gani, maamuzi yote tuliyofanya ya kisera yatakuwa na maana gani endapo watoto zaidi ya 27,000 ni watoto wengi sana kuwa nyumbani.”
Aidha, Mhe. Kairuki amesema kuwa masuala ya uandikishwaji wanafunzi na kuripoti kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza pia amekuwa akitumia kutafsiri utendaji wa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi.
“ Mimi hizi nazitafsiri kwenye maeneo mengi, ninyi mnaweza mkaona naangalia kwenye elimu peke, inanisaidia kutafsiri kuanzia Wakuu wa Willaya na pia naangalia Wakurugenzi tulionao, shida ni nini?
“ Haya ni maeneo mengine kati ya yale 12 ya mkataba wetu wa utendaji.”
Mhe. Kairuki amesema pia kwa upande wa ufaulu wa darasa la saba na kidato cha pili, bado Tanga haifanyi vizuri na kuwataka viongozi wajitafakari kilichotokea.
“Ndugu zangu tusipobadilika tutakuwa tunamvunja moyo Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali. Rais amechukua hatua mbalimbali za kitumishi kushughulikia changamoto nyingi na kuboresha sekta ya Elimu.
0 comments:
Post a Comment