METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, March 4, 2021

TUME YA MADINI YAFIKISHA ASILIMIA 75.8 UKUSANYAJI WA MADUHULI KWA MWAKA 2020-2021

Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa kuanzia kipindi cha mwezi Julai, 2020 hadi Februari 2021 katika mwaka wa fedha 2020-2021, Tume ya Madini ilifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 399.3 ikiwa ni sawa na asilimia 75.8 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 526.7.

Mhandisi Samamba ameyasema hayo leo tarehe 04 Machi, 2021 kwenye kikao chake na Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira iliyopo chini ya Tume ya Madini jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya ziara yake kwenye Kurugenzi na Vitengo kwa ajili ya kusikiliza na kutatua changamoto za utendaji kazi pamoja na kuweka mikakati ya ukusanyaji wa maduhuli na uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji kwenye Sekta ya Madini.

Amesema kuwa Tume ya Madini bado inaendelea kuweka mikakati ya kuzuia mianya yote ya utoroshaji wa madini, ukusanyaji wa maduhuli, uboreshaji wa masoko ya madini sambamba na usimamizi wa afya na mazingira kwenye migodi ya madini.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Samamba amewapongeza watumishi wa Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira kwa kazi nzuri ya usimamizi na ukaguzi wa mazingira na afya kwenye migodi ya madini hali iliyopelekea kupungua kwa ajali na athari za mazingira kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.

"Zamani kulikuwa na ajali za mara kwa mara kwenye migodi ya madini lakini kwa sasa ajali zimekuwa ni chache sana, hongereni sana na muendelee kuweka mikakati zaidi kwani nia yetu kama Serikali ni kuhakikisha watanzania wananufaika na rasilimali za madini pasipo kupata athari za aina yoyote," amesema Mhandisi Samamba.

Katika ziara yake, Mhandisi Samamba ameshatembelea Kurugenzi ya Leseni na TEHAMA na Kurugenzi ya Ukaguzi na Biashara ya Madini.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com