Na Mathias Canal, WEST-Rombo
Ukosefu wa heshima inaweza kuwa na hatari mbaya, kudhoofisha kabisa utume wa kufundisha na kujifunza. Katika miaka ya hivi karibuni, inaonekana kuwa nidhamu kwa walimu ni karibu haipo katika shule nyingi kote nchini na kama ipo inaendelea kushuka siku hadi siku.
Kufuatia hayo Wazazi/Walezi katika jamii nzima kwa ujumla wake wametakiwa kuendelea kuwathamini walimu kote nchini ili kuongeza ufanisi katika uwajibikaji.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 7 Januari 2023 Wakati akizungumza na walimu wakuu wa Shule za msingi na sekondari Wilaya ya Rombo katika mkutano uliofanyika kata ya Katangara Mrere.
Waziri Mkenda amesema kuwa Serikali imeendelea kuwekeza zaidi katika miundombinu ya elimu ikiwemo uwekezaji wa ujenzi wa Vyuo Vikuu nchini kwani wakati serikali inapata uhuru kulikuwa na vyuo vichache ukilinganisha na sasa.
Chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan, uwekezaji kwenye ujenzi wa shule na vyuo umeongezeka kwa kasi kubwa.
Kuhusu mageuzi ya elimu nchini, Waziri Mkenda amesema kuwa wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ipo katika mapitio ya sera na mitaala miongoni mwa mambo yatakayofanyiwa kazi itakuwa ni pamoja na kuhakikisha wanaoajiriwa ni wanafunzi wenye sifa zinazotakiwa.
Pia, Waziri Mkenda amesema kuwa serikali kwa sasa inaendelea na Ujenzi wa Kampasi mpya za Vyuo Vikuu katika mikoa 14 Tanzania pamoja na upande wa Zanzibar (Unguja na Pemba) katika maeneo ambayo hayana vyuo vikuu ukiacha vyuo huria.
Mikoa hiyo ambayo inatarajiwa kuwa na kampasi za vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini ni pamoja na Tabora, Katavi, Kigoma, Kagera, Singida, Manyara, Lindi, Rukwa, Mwanza, Simiyu, Tanga, Ruvuma, Shinyanga na Dodoma.
Waziri Mkenda amesema kuwa mwamko wa kufanya mageuzi ya elimu ni ajenda iliyopo duniani na kwamba Tanzania imewahi kuanza mageuzi hayo.
Prof.Mkenda amewapongeza wadau kwa namna wanavyoshiriki kikamilifu kutoa maoni yao madhubuti kwa ajili ya kusaidia mageuzi makubwa katika sekta ya elimu nchini.
“Baada ya Rais Samia kuingia madarakani alitoa maelekezo ya kufanya mapitio ya Sera na mabadiliko ya mitaala kwa lengo la kuhakikisha elimu inayotolewa inaendelea kuwa bora na kutoa elimu ujuzi. Niwaombe wadau tuendelee kushirikiana katika kuboresha na kukuza elimu nchini,” amesema Prof Mkenda.
Prof Mkenda amesema kuwa uamuzi wa Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutoa vishikwambi kwa walimu na wadhibiti ubora nchini utaleta mchango mkubwa katika kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya elimu nchini.
Vishikwambi hivyo takribani 300,000 vilivyotumika katika Sensa ya Watu na Makazi Agosti 23, mwaka huu, 293,400 vinagawiwa kwa walimu kwa lengo la kuboresha ufundishaji wanafunzi katika shule mbalimbali nchini.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment