METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, October 19, 2022

WALIOVAMIA MAENEO YA HIFADHI WAONYWA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula  akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji cha Lyamidati Mkoani Shinyanga wakati kamati ya mawaziri 8 wa kisekta wanaoshughulikia migogoro ya Ardhi ya Vijiji 975 walipofika katika eneo hilo

 

Sehemu ya wananchi waliohudhuria mkutano kati ya Kamati ya Mawaziri nane wa wizara za kisekta na wananchi wa kijiji cha Lyamidati Shinyanga.

Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Pindi Chanza  akizungumza katika mkutano wa hadhara  na wananchi wa kijiji cha Lyamidati Mkoani Shinyanga wakati kamati ya mawaziri 8 wa kisekta wanaoshughulikia migogoro ya Ardhi ya Vijiji 975 walipofika katika eneo hilo 

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Khamis Hamza Chillo   akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji cha Lyamidati Mkoani Shinyanga wakati kamati ya mawaziri 8 wa kisekta wanaoshughulikia migogoro ya Ardhi ya Vijiji 975 walipofika katika eneo hilo 

Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji cha Lyamidati Mkoani Shinyanga wakati kamati ya mawaziri 8 wa kisekta wanaoshughulikia migogoro ya Ardhi ya Vijiji 975 walipofika katika eneo hilo jana. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

 …………………………………..

Na Munir Shemweta, WANMM SHINYANGA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula amewaonya  wananchi walioingia kwenye migogoro ya matumizi ya ardhi na maeneo ya hifadhi nchini ambao maeneo yao yanafanyiwa tathmini na timu za wataalamu kutoongeza maeneo waliyopo  sasa.

Dkt Mabula alitoa kauli hiyo jana katika kijiji cha Lyamidati kilichopo kata ya Kadoto Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga  wakati Kamati ya Mawaziri nane wa Wizara za Kisekta wanaoshughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 walipotembelea mkoa wa Shinyanga.

Kijiji cha Lyamidati ambacho wananchi wake wameingia kwenye mgogoro wa matumizi ya ardhi  na eneo la hifadhi kinapakana na msitu wa hifadhi wa Nido ambapo baadhi ya vitongoji vipo ndani ya hifadhi huku uvamizi ukiwa kwenye maeneo ya makazi, kilimo pamoja na shughuli za ufugaji ndani ya hifadhi . 

Katika eneo hilo Kaya 78 kati ya 170 za kijiji chote zipo ndani ya msitu huku vitongoji 3 navyo vikiwa ndani ya hifadhi.

Maelekezo ya Kamati ya Mawaziri nane wa Wizara za Kisekta kwenye eneo hilo ni kufanyika tathmini ili vijiji ndani ya hifadhi virasmishwe, marekebisho ya mipaka yafanyike pamoja na kuandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula alisema. baada ya kumegwa kwa eneo lenye migogoro ya matumizi ya ardhi lazima mipaka ipitiwe upya ili kujua eneo la hifadhi na lile litakalo baki kwa ajili ya matumizi ya wananchi na kusisitiza kuwa jambo hilo wananchi wanatakiwa kuwa nalo kichwani.

” Hapo ulipo usisogeze mguu hata hatua moja mbele kutoka pale ulipo kuongeza eneo na kama una kishamba chako usiseme unaenda kuongeza shamba jipya kwa sababu utaratibu utataletwa na kufanyiwa mpango wa matumizi ya ardhi.

Alimsifia na kumshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa, pamoja na mabaya na uvamizi uliofanywa na wananchi  kwenye maeneo ya hifadhi bado ameagiza kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta kuzunguka na kuzungumza na wavamizi.

Mawaziri walioambatana na Dkt Mabula katika ziara hiyo, walisistiza umuhimu wa kuwepo mipango ya matumizi ya ardhi kwenye maeneo yaliyomegwa sambamba na maeneo ya hifadhi kutunzwa na kulindwa.

Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Pindi Chana aliwaambia wananchi kuwa, wizara yake inalo jukumu la kulinda. Kuitunza na kuihifadhi misitu yote nchini ambapo alisema hifadhi iliyoingia kwenye mgogoro wa matumizi ya ardhi katika kijiji cha Lyamidati Shinyanga ulishamegwa mara kadhaa hadi kubakia hekta 10,000.

Naye Waziri Ofisi ya Mazingira Muungano Khamis Hamza Chillo aliwahimiza wananchi kuhakikisha wanapanda miti sambamba na kujiepusha katika uharibifu wa vyanzo vya  maji.

Anthony Mavunde Naibu Waziri wa Kilimo alihimiza wataalamu kuhakikisha wanayawekea mipango ya matumizi ya ardhi maeneo yote yaliyomegwa ili kutengwa kwa ardhi kubwa kwa ajili ya shughuli za kilimo.

Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta imehitimisha ziara yake katika mkoa wa Shinyanga na sasa inaendelea mikoa ya Mwanza na Mbeya.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com