Na Mathias Canal, WEST-Dodoma
Serikali imeandaa mkutano maalumu kwa mara nyingine wa wadau wa
elimu kutoka maeneo na sekta mbalimbali nchini kote nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma leo tarehe 25
Septemba 2022 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda
amesema kuwa mkutano huo unatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 26 hadi 28
Septemba 2022 Jijini Dodoma.
Waziri Mkenda ameeleza lengo la Mkutano huo kuwa ni kujadili
Mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na Mabadiliko ya Mitaa ya Elimu
msingi.
Amesema kuwa Majadiliano hayo yatatokana na hatua iliyofikiwa na
mapitio hayo kupitia kamati maalumu zilizopewa majukumu hayo.
Waziri Mkenda amesema kuwa Mkutano huo unajumuisha,
Wahadhiri, Waajiri, Wadau wa Maendeleo, Taasisi za umma na Binafsi, Taasisi za
Dini, Taasisi zinahusika na uendelezaji wa lugha, Wabunge, Wajumbe toka
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Taasisi zisizo za Kiserikali, Jumuiya za
kitaaluma, na Taasisi za Sayansi na Utafiti.
Katika hatua nyingine, Waziri Prof Mkenda amesema kuwa tarehe 27
Septemba, 2022 serikali itatangaza rasmi majina ya wanafunzi Waliofaulu kwa
kiwango kikubwa katika masomo ya Sayansi hivyo wanastahili kupata ufadhili wa
SAMIA SCHOLASHIPS endapo watadahiliwa kusoma masomo ya Sayansi, Elimu tiba na
Uhandisi kwenye vyuo mbalimbali ndani ya nchi.
"Mtakumbuka Wizara yetu ilitoa ahadi kupitia hotuba ya
bajeti ya kuanzisha programu mpya ya kutoa ufadhili wa masomo ya elimu ya juu
kwa wahitimu bora wa kidato cha sita katika masomo ya Sayansi ambapo mpaka sasa
tuna majina karibu 600 ya wanafunzi ambao wamepata ufaulu wa kiwango kikubwa
katika masomo hayo" Amekaririwa Waziri Mkenda
Kadhalika, Waziri Mkenda ameukumbusha umma kuwa serikali
imezindua tuzo za waandishi bunifu zijulikanazo kama Tuzo za Mwalimu Nyerere,
hivyo ameendelea kukaribisha Waandishi Bunifu wa Riwaya na Mashairi kuwasilisha
maandiko yao ili kuwania tuzo hizo.
Prof Mkenda amesema kuwa Mwisho wa kupokea Mawasilisho hayo ni Novemba 30, 2022 ambapo kwa taarifa zaidi kuhusu tuzo hizo na maulizo wanaweza kufuatilia katika akaunti maalumu za mitandao ya kijamii za tuzo Nyerere au mitandao na tovuti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Taasisi ya Elimu Tanzania-TET kwa anuani ya tuzonyerere@tie.go.tz
MWISHO
0 comments:
Post a Comment