Na Mathias Canal,
WEST-Morogoro
Serikali imesema kuwa
inaendelea kufanya mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na
mabadiliko ya mitaala ili kuongeza ubora wa elimu na mafunzo.
Katika Mapitio hayo ya
mitaala na sera pia yanaangazia kwa karibu Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ili
wakati utatuzi wa changamoto ukiendelea serikali kuangalia nini kifanyike ili
kuboresha elimu ujuzi kwa wanafunzi ikiwemo watu wazima.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo leo tarehe 9 Septemba 2022
wakati wa hafla fupi ya ufungaji wa mafunzo ya Baraza la Usimamizi wa Taasisi
ya elimu ya watu wazima (TEWW) Kampasi ya Morogoro.
Prof Mkenda amesema kuwa
Taasisi hiyo inapaswa kushiriki kikamilifu katika utoaji wa maoni ikiwa ni
pamoja na kushirikisha kwa karibu wadau wengine kutoa maoni namna ya kuboresha
taasisi hiyo hususani katika maeneo ya ujuzi.
Pia, Prof Mkenda amesema kuwa
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa kuhusu kuhakikisha
kuwa watanzania waliokosa fursa ya kusoma kutokana na matatizo mbalimbali
wanapata fursa ya kuendelea na masomo.
Serikali itaendelea kuisaidia
Taasisi ya elimu ya watu wazima ili kuratibu na kusimamia vyema urahisi wa
wananchi kupata fursa ya elimu, hivyo ili kukamilisha jambo hilo itaendelea
kuimarisha miundombinu ikiwemo ukarabati na ujenzi wa majengo ya taasisi.
"Majengo ni muhimu
lakini Elimu sio majengo pekee tunaweza kutumia muda mrefu kwenye majengo,
serikali italeta hela kwa ajili ya majengo lakini kama hatukuweka weledi kwa
watu hatuwezi kufika" Amekaririwa Waziri Mkenda
Waziri Mkenda amemtaka
Mwenyekiti wa Baraza hilo pamoja na wataalamu kufanya ziara nchini Ujerumani
ili kujionea namna Taasisi ya elimu ya watu wazima nchini humo inavyofanya kazi
ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la
usimamizi wa (TEWW) Dkt Naomi Katunzi amempongeza waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda kwa usimamizi madhubuti wa baraza hilo pamoja
na mabadiliko makubwa ya iutendaji yanayofanyika katika wizara.
Amesema kuwa Mafunzo hayo
yanayotolewa chini ya Chuo cha Uongozi pamoja Ofisi ya Msajili wa hazina
yamejikita katika kuwaongezea ufanisi wa kiutendaji na uwajibikaji serikali
ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa wanaacha alama na kielelezo bora katika
uwajibikaji.
Mwenyekiti huyo amezitaja
changamoto zinazoikabili taasisi hiyo kuwa ni pamoja na ukarabati wa majengo
chakavu ikiwa sambamba na ujenzi wa majengo mapya kwa ajili ya ofisi.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment