Na
Mathias Canal, WEST-Dodoma
Kamati ya Huduma na Maendeleo
ya jamii imempongeza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf
Mkenda kwa kusimamia kwa weledi na ufanisi uratibu wa zoezi la watumishi
kuhamia Jijini Dodoma kuitikia maelezo ya serikali.
Kauli hiyo ya pongezi
imetolewa leo tarehe 8 Septemba 2022 na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe Stanslaus
Nyongo (Mb) wakati kamati hiyo ilipotembelea na kukagua ujenzi wa Ofisi za Tume
ya Nguvu za Atomiki (TAEC) Jijini Dodoma.
Mwenyekiti Nyongo amesema
kuwa Wizara hiyo imetii kwa vitendo maelekezo ya serikali ya kuhamia Dodoma
ambayo ni maelezo muhimu yaliyotolewa na serikali.
Mhe Nyongo amesema kuwa
kujengwa kwa ofisi na kuhamia Jijini Dodoma kutarahisisha wananchi kupata
huduma kwa urahisi na ukaribu kwani huduma hiyo ni muhimu kwa Usalama wao na
usalama wa Taifa kwa ujumla.
“Sisi kama kamati tumeridhika
kwa kuja na kuona na tunaahidi tutakuja tena kujionea kazi zinazofanywa pindi
jengo litakapoanza kutumika” Amekaririwa Mhe Nyongo
Mwenyekiti huyo ameitaka
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhakikisha kuwa inawatangazia wananchi
kwa kila hali ili waweze kujua kuwa huduma zimerahisishwa na tayari
zinapatikana makao makuu ya nchi.
Kwa upande wake Waziri wa
Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda amesema kuwa ziara hiyo ya
kamati ya Bunge kuangalia ujenzi wa ofisi za kitaifa za Tume ya Nguvu za
Atomiki (TAEC) imefikia hatua nzuri za ujenzi na hiyo ni sehemu muhimu katika
utekelezaji wa maelekezo ya serikali kuhamia Jijini Dodoma.
Waziri Mkenda amesema kuwa
utekelezaji huo wa maelekezo ya serikali unaenda sambamba na ujenzi wa majengo
ya Taasisi za Wizara ili wafanyakazi wanapohamia Dodoma wawe na sehemu ya
kufanyia kazi na Taasisi isikodi sehemu ya kuafanyia kazi.
Kadhalika amempongeza
Mtendaji Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomoki Prof Lazaro kwa utekelezaji mzuri wa
ujenzi wa Ofisi Jijini Dodoma ambao umefikia asilimia 85
MWISHO
0 comments:
Post a Comment