METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, September 9, 2022

DKT. KIRUSWA AIAGIZA GST KUFANYA UTAFITI WA CHUMVI MANYONI











Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kufanya tafiti za madini katika vijiji vya Kinangali, Majili, Mpandagani na Mahaka ili kutambua kiasi na ubora wa chumvi iliyopo katika vijiji hivyo kwa lengo la kuitangaza fursa hiyo ili kuwavutia wawekezaji.

Dkt. Kiruswa ametoa maagizo hayo baada ya kutembelea eneo la uchimbaji wa madini ya chumvi lililopo katika kijiji cha Kinangali Kata ya Majili wilayani Manyoni mkoa wa Singida.

"Naomba nitumie fursa hii kumuagiza Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba ambaye nimeambatana naye hapa kuleta wataalamu wake kupima katika eneo hili ili kujua kiasi gani cha chumvi kilichopo hapa na ubora wake, itakuwa rahisi kwetu kuitangaza ili tuwavutie wawekezaji wakubwa," amesema Dkt. Kiruswa.

 Aidha, Dkt. Kiruswa amemuagiza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida Chone Malembo kuhakikisha anashirikiana na uongozi wa kijiji, wachimbaji na wafanyabiashara wa chumvi ili kupata bei elekezi ya madini hayo na kuhakikisha wanauza kwa kutumia kipimo cha mizani ambapo kwa sasa kinatumika kipimo cha debe katika vijiji hivyo baada ya kugundua kuwa wachimbaji wadogo wa Chumvi wanapunjwa bei.

Sambamba na hayo, Dkt. Kiruswa amemtaka Malembo kuendelea kutoa elimu ya mazingira na uchimbaji salama kwa wachimbaji wadogo wa madini ya chumvi na pia, kutoa elimu ili kujiunga katika vikundi ambapo itasaidia kuweza kukopesheka.

Kwa upande wake, Mbunge wa Manyoni Mashariki Dkt. Pius Chaya amempongeza Dkt. Kiruswa kwa kutembelea shughuli za uzalishaji wa chumvi ambapo changamoto zilizotolewa za bei, kiasi cha chumvi na ubora wake zinaenda kutafutiwa suluhisho la kudumu.

Naye, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Dkt. Mussa Budeba ameahidi kupeleka wataalamu wake ili kufanya tafiti kwa lengo la kugundua kiasi na ubora wa madini ya chumvi yaliyopo katika vijiji vya Kinangali, Majili, Mpandagani na Mahaka wilayani Manyoni.

Mkoa wa Singida umebahatika kuwa na aina nyingi za madini ikiwa ni pamoja na madini ya metali kama vile dhahabu na shaba, madini ya ujenzi kama vile, jasi, mchanga na kifusi na madini ya viwandani kama vile chumvi.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com