METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, August 16, 2022

KANISA LIMETAKIWA KUENDELEA KUHUBIRI NA KUFUNDISHA NENO LA MUNGU KWA UAMINIFU HATA MWISHO








Maganga Gwensaga – Dodoma

Wakristo nchini wametakiwa kuendelea kuhubiri kweli ya Mungu ambayo ni Neno la Mungu , huku wakiyazingatia maelekezo yote yanayopatikana katika Maandiko Matakatifu yanayotolewa na watumishi wake na  kuyashika kikamilifu.

Agizo hilo limetolewa na Askofu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Mpwapwa Dinare ya Kongwa Dkt. Jacob Erasto Chimeledya wakati akitoa ujumbe wa Neno la Mungu katika ibada ya kipaimara iliyofanyika Agosti  14, 2022 kanisani hapo.

Katika ibada hiyo iliyoambatana na uzinduzi wa Jengo la kuabudia,  Askofu Chimeledya alisema  kanisa la sasa linatakiwa kuzingatia maelekezo yote yaliyofundishwa na mitume kupitia maandiko matakatifu ili waweze kutoyafuata mafundisho ya uongo, kama ambavyo waumini wa kanisa la kwanza walivyokengeuka na kufuata mafundisho ya uongo.

“ Kuna tatizo lilitokea katika kanisa la kwanza pale Efeso waumini wake walifuata walimu wa uongo na kwa makundi makundi  wakaanza kuiamini ile imani na Timotheo alikuwa peke yake, na kundi kubwa la watu walijitenga na kweli ya Mungu wakiamini mafundisho ya uongo na kuzifuata roho zidanganyazo.” Alisema Askofu

Alisema kanisa linaweza kufa endapo tu waumini hawatozingatia maagizo ya Mungu kama ambavyo Paulo alimwambia Timotheo akitolea mfano wa Mataifa ya Uingereza, Marekani, Australia  ambapo baadhi ya Majengo hayatumiki tena kama sehemu za kuabudia  yamegeuka kuwa Migahawa  baada ya waumini kusikiliza mafundisho ya Duniani, wakayazingatia, wakayaamini na kuyafuata  hayo na kuacha kweli ya Mungu.

“ Ndugu zangu tunaambiwa na sisi kuwa utafika wakati watu wataikataa hiyo kweli ya Mungu, Watakupinga,  watakwambia wewe muongo nenda zako, unatudanganya kila siku, kwanza unatuchelewesha, Mtume  Paulo anamwandikia Timotheo anasema itafika wakati watu watayakataa mafundisho yenye uzima ila watazifuata nia zao wenyewe watajipatia walimu makundi makundi kwa kuwa wana masikio ya utafiti watajiepusha wasisikie yaliyo kweli watageukia hadithi za uongo.” Aliongeza Askofu

Aliwataka Wakristo kuzingatia mambo matatu muhimu katika utumishi wao akiwahimiza kuwa watoaji iwe ni kwa mali, maisha  au miili yao lakini pia wasiache kumwamini Yesu Krito , kuwa na matumaini nae na kusimama katika kweli kwenye  maisha yao yote  wawapo hapa Duniani.

Katika Risala yao kwa Askofu Chimeledya waumini wa kanisa hilo walimpongeza kwa kazi nzuri aliyoianzisha katika kipindi chake cha Uaskofu zikiwemo kuhimiza Semina na Mikutano ya Kiroho, kuwatunza viongozi wastaafu, Kuanzisha Ibada za Jumuia, Ujenzi wa Makanisa na nyumba za watumishi.

Ibada hiyo ilienda sambamba na kuwekewa mikono wana Kipaimara wa Dinare ya Kongwa wapatao 143, ambapo viongozi mbalimbali wa Serikali na Chama cha Mapinduzi walihudhuria akiwemo Spika Mstaafu na Mbunge wa Kongwa Mhe. Job Ndugai, Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. White Zuberi  Mwanzalila na Katibu  wa CCM Wilaya hiyo Joyce Mkaugala.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com