Mwenyekiti wa
kamati ya sensa wilaya ya kongwa Mkoani Dodoma ambaye pia ni Mkuu wa wilaya hiyo Mhe. Remidius Mwema, amewataka
wakufunzi wa sensa wilayani humo
kufahamu kwamba serikali imewaamini kusimamia
zoezi kubwa lililo mbele la kuwafundisha
makarani, wasimamizi wa maudhui na wasimamizi wa Tehama
akiwataka kufanya kazi wakitaguliza uzalendo mbele.
Mhe. Mwema amesema hayo Julai 28, 2022 wakati
akizungumza na timu ya wakufunzi hao zikiwa ni siku chache kabla ya kuanza kwa
mafunzo kwa makarani, wasimamizi wa maudhui na wasimamizi wa Tehama
yanayotarajia kuanza tarehe 31 Julai mpaka tarehe 19 Agosti mafunzo
yatakayoendeshwa na wakufunzi hao.
Muamini kwamba mmeaminiwa na wilaya ya kongwa
tunajivunia uwepo wenu tukiamini kwamba zoezi litaenda vizuri, tunaamini
mtaenda kuwa mstari wa mbele na mkumbuke yale yote mliyojifunza na yatakuwa na tija endapo tu mtayafanyia kazi.
Alisema Mhe. Mwema
Amewataka wakufunzi hao kutambua kwamba wamebeba
dhamana kubwa ya nchi na kwamba tukio
hili ni zoezi la kitaifa kila mmoja ana
wajibu wa kulinda na kuhakikisha kwamba jambo hili analikamilisha kikamilifu.
Tuna matarajio makubwa kwenu na tusingependa
litokee doa lolote na Kwa kuwa mnaenda kuwafundisha wengine hakikisheni
mnazingatia msingi ya ualimu muende kusimamia miongozo nasi kama kamati ya wilaya tutashirikiana bega kwa bega kuhakikisha tunafanikisha zoezi hili.
Aliongeza Mhe. Mwema
Kwa upande wao wakufunzi hao wamesema wamejiandaa na
kujipanga vizuri na wako tayari kuanza kazi na wamemhakikishia Mwenyekiti
kwamba kwa mafunzo waliyoyapata na mbinu walizopewa na walimu wao kila kitu kitaenda sawa.
Mafunzo kwa makarani wa sensa, wasimamizi wa maudhui
na wasimamizi wa Tehama wapatao 205,000 yatafanyika katika ngazi ya Wilaya
kuanzia tarehe 31 Julai hadi tarehe 18 Agosti.
Aidha washiriki wengine wa mafunzo katika ngazi za Wilaya ambao watashiriki katika siku mbili za Mwanzo, yaani tarehe 31 Julai, 2022 na tarehe 1 Agosti, 2022 ni watendaji wa kata wote nchini kwa Tanzania Bara na Masheha wote wa Tanzania Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment