METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, August 5, 2016

Polisi Wamnyima Tundu Lissu Dhamana, Atupwa Rumande


JESHI la Polisi, kanda Maalumu ya Dar es Salaam limemnyima dhamana, Tundu Lissu, Mwanasheria Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), baada ya kumaliza kuhojiwa katika kituo kikuu cha polisi.

Baadhi ya viongozi waliofika kumwekea dhamana  ni pamoja na  Freeman Mbowe Mwenyekiti wa Chadema, Edward Lowassa Waziri Mkuu wa zamani na mjumbe wa kamati kuu wa Chama hicho, aliyefika saa 12:14 jioni akiungana na viongozi na wanachama wa chama hicho.

Baada ya kufika Lowassa wanachama na wafuasi wa Chadema waliokuwa nje ya ofisi hizo za polisi walianza kuimba wimbo wa kumuita rais, rais, rais ikiwemo na kauli mbiu ya maarufu ya Peoles power.

Mara baada ya kufika alipokelewa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe aliyekuwa amepanda gari moja na Meya wa Kinondoni, Boniface Jacob waliokuwa nje ya geti.

Viongozi hao waliokuwa nje baada ya kuzuiwa kuingia ndani na polisi waliongozana na Lowassa kuomba kuingia lakini walizuiwa hali iliyofanya wachukue uamuzi wa kuondoka.

Kiongozi aliyeruhusiwa kuingia alikuwa ni Meya wa Dar es Salaam, Isaya Mwita.

Akizungumzia kuhusu hilo, Peter Kibatala mwanasheria wa Lissu alisema kwamba mahojiano kati ya jeshi hilo na mtuhumiwa yalianza saa 9:30 hadi saa 12:30.

“Katika maelezo ya polisi wanasema kwamba wakati Lissu akitoka mahakamani juzi kwenye kesi yake  alitamka maneno ya uchochezi, lakini haya yote yanahitaji ushahidi,” alisema Kibatala.

Wakili huyo alisema kwamba polisi baada ya kumaliza mahojiano na wao wakiwa wameandaa utaratibu wa dhamana walikataliwa hadi leo Ijumaa atakapofikishwa mahakamani.

Aliyesambaza Ujumbe Asakwa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida,   Thobias Sedoyeka  ametangaza kumsaka mtu aliyesambaza ujumbe ambao amaedai “una ishara zote za uchochezi” unaoonyesha umeandikwa na Lissu   baada ya kukamatwa na jeshi hilo.

Alisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa kina kwenye mitandao ya  jamii kuhusu ujumbe huo.

Ujumbe huo ambao pia umenukuliwa na jeshi hilo katika taarifa yake, ulieleza jinsi polisi mkoani Singida walivyomkamata Lissu baada ya kumaliza mkutano wake wa hadhara   huku akihamasisha watu kutokubali kunyamazishwa na “Udikteta Uchwara”.

“Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina kwenye mitandao ya  jamii kuhusu ujumbe mfupi wa maneno uliosambazwa katika mitandao hiyo baada ya kukamatwa kwa Lissu ukiwa na ishara zote za uchochezi…,” alisema Sedeyoka na kuongeza:

“Katika uchunguzi huo endapo mtu yeyote atabainika kutuma taarifa hiyo basi Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali za  sheria zinazostahili ikiwamo kumkamata na kuwafikisha mahakamani mara moja.”

Ujumbe huo ulisomeka, “Wakubwa sana salamu. Ninawaandikieni maneno haya nikiwa chini ya ulinzi wa polisi Singida. Nimemaliza kuhutubia mkutano  wa hadhara mji mdogo wa Ikungi ambao ni makao makuu ya jimbo la Singida Mashariki.

“Mara baada ya kushuka jukwaani nilifuatwa na RCO wa mkoa aliyejitambulisha kwa jina la Babu Mollel na kuniarifu kuwa ameelezwa na RPC nikamatwe. Wakati huohuo, kuna amri ya kunikamata iliyotoka Dar es Salaam kwa hiyo nipo nguvuni ninasubiri maelekezo ya wanapotaka kunipeleka…

“Its likely (kuna uwezekano) nitasafirishwa Dar usiku huu. Infact ni usiku huu kwa taarifa za sasa hivi. Kwa vyovyote itakavyokuwa ‘there is no turning back’ (hakuna kurudi nyuma), there is no shutting up (hakuna kufunga mdomo). Nitapambana kutetea haki yetu ya kuwasema watawala popote nitakapokuwa.

“Whether in freedom or in jail as long as I have a voice to speak with. (Nikiwa huru au kifungoni ilimradi nina sauti ya kuzungumza) sitakubali kunyamazishwa na Dikteta Uchwara. Msikubali kunyamazishwa na Dikteta Uchwara. Aluta continua!!!! From Tundu Lissu”.


Kamanda Sedoyeka  alisema endapo itathibitishwa kuwa Lissu ndiye aliyeandika na kusambaza ujumbe huo ataingia tena matatani kwa kukamatwa na kuchukuliwa hatua za  sheria kama lilivyoeleza jeshi hilo.

Hiyo ni mra ya tatu kukamtwa kwa mbunge huyo kwa kipindi cha miezi michache na    amekwisha kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za uchochezi.

Kesi ya kwanza ni ile iliyodaiwa ametoa lugha ya uchochezi katika habari iliyochapishwa na gazeti la Mawio na kesi ya pili ni   ya kutoa maneno ya uchochezi kwa kumwita Rais Magufuli ‘Dikteta Uchwara’
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com