Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kutoa Tamko la Serikali katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni Duniani, leo Jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Mazingira Dkt. Andrew Komba (kushoto) akifuatilia Mkutano wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo (hayupo pichani) wakati akizungumza na waandishi wa habari na kutoa Tamko la Serikali katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni Duniani leo Jijini Dodoma.
Na Lulu Mussa,Dodoma
Serikali imesema Itifaki ya Montreal imepata mafanikio makubwa kwa kupunguza takribani asilimia 98 (takribani tani 1.8) ya uzalishaji wa matumizi ya kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Hewa ya Ozoni na kuchangia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Haya yamesemwa hii leo Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo wakati akitoa tamko la Serikali katika kuadhimishia Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni Duniani.
Amesema baadhi ya kemikali zinazomong’onyoa tabaka la Ozoni pia husababisha kuongezeka kwa joto duniani na matokeo ya tafiti yanathibitisha kwamba kiwango cha kemikali zinazoharibu tabaka la Ozoni angani kinaendelea kupungua na inakadiriwa kuwa iwapo jitihada za utekelezaji wa Itifaki hii zitaendelea, Tabaka la Ozoni litarudi katika hali ya kawaida ifikapo katikati ya karne hii.
Waziri Jafo amesema katika jitihada za kuhifadhi Tabaka la Ozoni, mwaka 1996, Serikali iliandaa na kutekeleza Programu ya Taifa ya kuondosha matumizi ya kemikali zinazomong’onyoa tabaka la ozoni ili kuhakikisha kwamba hakuna sekta ya uchumi au jamii inaathirika kutokana na matakwa ya Itifaki ya Montreal. Aidha, programu hii ilianzisha utaratibu wa kusimamia na kudhibiti uingizaji wa kemikali na bidhaa zenye kemikali zinazoharibu tabaka la Ozoni kutoka nje ya nchi.
Waziri Jafo, ameikumbusha jamii wajibu wa kuendelea kulinda tabaka la ozoni kwa kuepuka kuingiza nchini kemikali na vifaa vinavyotumika kumong’onyoa tabaka la ozoni kama vile majokofu na viyoyozi vilivyokwishatumika (mtumba) bali kuingiza nchini vipoozi mbadala na rafiki kwa tabaka la Ozoni.
“Natoa rai kwa jamii kununua bidhaa zilizowekwa nembo ya “Ozone friendly” yaani ‘sahibu wa Ozoni’ au “CFC-free” ikiashiria haina wala haikutengenezwa na kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni, kuepuka kutupa ovyo majokofu ya zamani ama vifaa vya kuzima moto vyenye kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni” Alisisitiza Waziri Jafo.
Waziri Jafo amebainisha kuwa, Serikali imeandaa na kutekeleza Programu ya Taifa ya kuondosha matumizi ya kemikali haribifu ambayo ni pamoja na kuandaa Kanuni za Usimamizi wa Kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la hewa ya Ozoni, kutoa mafunzo kwa mafundi mchundo 500 wa viyoyozi na majokofu kuhusu njia bora za kuhudumia vifaa hivyo bila kuathiri Tabaka la hewa ya Ozoni na Kusambazwa kwa Vitambuzi vya kemikali hizi vipatavyo 18 katika vituo vya mipakani.
Kaulimbiu inayoongoza maadhimisho ya mwaka huu ni Mkataba wa Montreal: Tulinde Afya ya Binadamu, Hifadhi ya chakula na kuhakikisha chanjo za Uviko 19 ni salama” Ujumbe wenye lengo la kukumbusha Jumuiya ya Kimataifa utekelezaji wa Itifaki ya Montreal katika udhibiti wa kemikali zinazomong’onyoa tabaka la ozoni kwa kumeweka mifumo thabiti ya kuhakikisha afya ya binadamu na mazingira zinalindwa ikiwemo tabaka la ozoni.
Vilevile, ujumbe huu unazikumbusha nchi wanachama wa Itifaki ya Montreal kuhakikisha kemikali mbadala (gesi) zinapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu ili kuchangia katika hifadhi ya chakula na jitihada za kupambana na janga la maambukizi ya Ugonjwa wa virusi ya Korona (UVIKO – 19) katika kuhakikisha kuwa chanjo zinakuwa salama.
Ozoni ni tabaka la hewa lililopo kwenye angahewa ya juu, takribani kilometa 15 hadi 30 juu ya ardhi likiwa na kazi ya kuchuja kiwango kikubwa cha mionzi ya jua isifike kwenye uso wa dunia.
0 comments:
Post a Comment