Na
Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
WAZIRI wa Kilimo Prof Adolf Mkenda amesema kwa sasa mahindi yatanunuliwa tani 90,000 ambapo Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) utaanza kununua kwenye mikoa saba kwa bei ya sh. 500 kwa Kilogramu huku Bodi ya nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) ikinunua mikoa sita kwa bei ya soko.
Alitaja mikoa saba ambayo NFRA itaanza kununua mahindi hayo kuwa
ni pamoja na Ruvuma, Rukwa, Njombe, Songwe, Mbeya, Katavi na Iringa huku CPB
ikinunua mikoa sita ambayo ni Rukwa, Katavi, Njombe, Songwe, Dodoma na Manyara.
Hayo ameyasema jijini Dodoma leo tarehe 14 Septemba 2021 wakati
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua zilizochukuliwa mara baada ya
Rais Samia Suluhu Hassan kutoa Tsh Bilioni 50 kwa ajili ya kuiwezesha NFRA
kununua mahindi kwa wakulima hasa wadogo.
Amesema zoezi la kununua mahindi tayari lilitangazwa na Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa mara baada ya Rais Samia kuidhinisha sh. Bilioni 50 kwa
kazi hiyo.
Amebainisha kuwa mwaka huu zimezalishwa tani milioni sita za
mahindi huku ziada ikiwa mara mbili ya uzalishaji uliofanyika kwa mwama
uliopita huku nchi za Zimbabwe, Zambia zikitajwa kuzalisha kwa wingi nafaka
hiyo.
“Lazima tutoe tahadhari kwa maana mwakani bei inaweza kupanda
lakini kwakuwa kuna mikoa inaongoza kwa uzalishaji hapa nchini kama Ruvuma ikifuatiwa
na Rukwa bei ni ndogo sana wakati mkoa wa Katavi, Songwe zikiwa chini zaidi
hali inayompeleka mkulima kushindwa kupata fedha za kujikimu na kujiandaa kwa
msimu ujao”
“Tayari NFRA wamepewa fedha za kununua na tayari zimeanza
kuingia hizi ni fedha za serikali zilitolewa kwa kazi hiyo hivyo NFRA wataanza
kununua mahindi katika mikoa saba huku CPB ikinunua mikoa sita,” Amekaririwa
Waziri Mkenda
Amesema mahindi hayo yatanunuliwa kupitia Vyama cha Ushirika wa Kilimo na
Masoko (AMCOS) au vikundi vya wakulima vilivyosajiliwa na kwa wakulima wadogo
kwa magunia yasiyozidi 300 au tani 30 kwakuwa wanataka rekodi ya kila mkulima
aliyelima mahindi yanunuliwe na fedha zilizotolewa na Serikali zitumike kama
ilivyokusudiwa.
Amesema baada ya zoezi hilo kufanyika wizara itafanya
ufuatiliaji kwa viongozi wa mikoa ili kupata taarifa na namna mgawanyo wa
ununuzi ulivyofanyika kwenye mikoa tajwa.
“Tutakagua hivyo wananchi au wakulima mkiona dalili za ukiukwaji
wa ununuzi wa mahindi toeni taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo
kwenye maeneo yenu,” amebainisha.
Afisa Mtendaji Mkuu NFRA, Milton Lupa amesema wanaenda kununua
nafaka hiyo katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwenye mikoa ya Songea,
Ruvuma, Songwe, Njombe, Katavi na Rukwa kupitia AMCOS na wakulima
waliosajiliwa.
“Wananchi watulie tutanunua mahindi, wapunguze vurugu kwakuwa
tutafuata utaratibu uliowekwa tunawahakikishia tutawafikia wakulima wenye
kipato cha chini wenye mahindi yanayokidhi vigezo,” amesema.
Naye Mkurugenzi Mkuu CPB, Dkt Anselim Moshi amesema watanunua
mahindi hayo kama walivyoelekezwa na wizara na kwamba wameshaanza kutafuta
masoko nje ya nchi mbalimbali zikiwemo Kenya, Sudani Kusini,
Comoro, Burundi na Rwanda.
“Tumetafuta fedha kwa kukopa kwenye benki tutanunua nafaka hiyo
kwa wingi na kusafirisha nje ya nchi ambapo ndio tumetafuta masoko kwa ajili ya
kuuza, ”amesema.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment