Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na viongozi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI kwenye jengo la Mkapa jijini Dodoma, Mei 31, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na viongozi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI kwenye jengo la Mkapa jijini Dodoma, Mei 31, 2022. Kulia kwake ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Innocent Bashungwa.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Nchi (OR-TAMISEMI), Innocent Bashungwa na viongozi wengine wa wizara hiyo wahakikishe kuwa suala la ukusanyaji mapato kwenye Mikoa, Halmashauri na Mamlaka za Serikali za Mitaa linapewa kipaumbele ili kuongeza mapato ya Serikali.
“Ajenda ya ukusanyaji mapato iwe ya kudumu ili yaongezeke hadi kufikia shilingi trilioni 2 kutoka makadirio ya sasa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo Halmashauri zimekadiria kukusanya mapato ya ndani ya shilingi trilioni 1.01 ikilinganishwa na shilingi bilioni 863.85 zilizoidhinishwa kwa mwaka 2021/2022,” amesema.
Ametoa wito huo leo (Jumanne, Mei 31, 2022) alipokutana na Waziri wa TAMISEMI, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu pamoja na Wakurugenzi na Wakuu wa taasisi za wizara hiyo kwenye kikao alichokiitisha jijini Dodoma ili kuwakumbusha wajibu wao.
“Nimekuja kwenye ziara ya kawaida ya kiutendaji ili kuzungumza na viongozi wakuu wa wizara na wakuu wa idara. Ni lazima ujitambue wewe ni nani hapa kwenye wizara, unatakiwa kufanya nini, mpango kazi wako ukoje na je ni wako peke yako ama unahitaji watu wengine ili uweze kuutekeleza,” amesema.
“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anataka kuona Watanzania wanafikiwa na huduma. Ni lazima tujiulize, je huduma hizo zinafika kwa wananchi kwa wakati. Watanzania wanaitegemea TAMISEMI kuanzia ngazi ya mkoa, wilaya, halmashauri, kata vijiji hadi vitongoji. Kwa hiyo, tunapaswa kuhakikisha hiyo chain inafanya kazi,” amesema.
Amesema watumishi hao wanapaswa kutambua kwamba bila uaminifu, uadilifu na uwajibikaji hawawezi kufanikiwa lakini pia wanapaswa kusimamia mambo hayo matatu hadi ngazi za chini
Amewapongeza viongozi na Watendaji wa wizara kwa kufanikiwa kuongeza hati safi kwenye taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) katika kipindi cha mwaka 2019/2020 na 2020/2021.
“Taarifa ya CAG kuhusu Hesabu za Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mwaka wa fedha 2020/2021 imebainisha Halmashauri 178 sawa na asilimia 96 zimepata hati safi, Halmashauri sita sawa na asilimia tatu zimepata hati zenye shaka na Halmashauri moja sawa na asilimia moja imepata hati mbaya”.
Waziri Mkuu amesema matokeo ya ukaguzi wa hesabu za mwaka wa fedha 2020/2021 yanaonesha mwenendo mzuri wa aina ya hati za ukaguzi zilizotolewa ikilinganishwa na ukaguzi wa hesabu za mwaka wa fedha wa 2019/2020 ambapo Halmashauri zilizopata hati safi zilikuwa 124 sawa na asilimia 67, Halmashauri zilizopata hati zenye shaka zilikuwa 52 sawa na asilimia 29 na Halmashauri zilizopata hati mbaya zilikuwa nane sawa na asilimia nne.
“Mwaka huu hati mbaya zimepungua kutoka nane hadi moja, kwa hiyo kama leo tumefikia asimilia 96 tuna uwezo wa kufikia asilimia 100, kutafuta ile mbaya na zenye mashaka sita zikaondoka.”
Ameitaka menejimenti ya wizara hiyo iwe na ubunifu, iongeze matumizi ya TEHAMA ili kuongeza mapato ya Serikali, Wakuu wa Idara wagawe majukumu kwa wasadizi wao na wakurugenzi wawe na vikao vya mara kwa mara na wasaidizi wao.
0 comments:
Post a Comment