Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Zainab Chaula akizungumza wakati akifungua Mkutano wa wadau wa NGOs kwa kanda ya Kati katika mkutano uliolenga kukusanya maoni kuhusu Mkakati wa Kitaifa wa Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali uliofanyika jijini Dodoma
Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Vickness Mayao akieleza namna Ofisi yake inavyoratibu zoezi la kukusanya maoni kuhusu Mkakati wa Kitaifa wa Uendelevu wa NGOs nchini katika mkutano uliofanyika jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa kikosi kazi cha kukusanya maoni kuhusu mkakati wa uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Nensia Mahenge akielezea namna Kikosi hicho kinavyoendelea kukusanya maoni kuhusu Mkakati wa Kitaifa wa Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali wakati wa Mkutano wa kutoa maoni juu ya Mkakati huo uliofanyika jijini Dodoma.
Baadhi ya wadau wa NGOs wakifuatilia mkutano wa Kanda ya Kati wa kukusanya maoni kuhusu Mkakati wa uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika mkutano uliofanyika jijini Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Zainab Chaula akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali mara baada ya kufungua mkutano wa wadau hao wa kutoa maoni kuhusu Mkakati wa uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Mkutano huo umefanyika jijini Dodoma Mei 20, 2022
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WMJJWM
Na WMJJWM Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) nchini kuhakikisha malengo yao na vipaumbele vinaendana na mahitaji ya jamii ikiwemo Mpango wa Taifa wa Maendeleo.
Dkt.Chaula ametoa kauli hiyo jijini Dodoma Mei 20, 2022 wakati akifunga mkutano wa wadau wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali uliolenga kukusanya maoni kuhusu Mkakati wa Kitaifa wa Uendelevu wa NGOs kwa Kanda ya Kati.
Dkt. Chaula alisema kuwa Serikali inaendelea kuratibu Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili yaweze kufanya kazi zake kwa kuzingatia Sheria Kanuni na taratibu zilizopo ili kuwahudumia wananchi na miradi wanayotekelezwa ilete manufaa na faida kwa wananchi hasa waliopo katika ngazi ya vijiji.
Katika hatua nyingine Dkt. Chaula ametumia nafasi hiyo kuyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutoa maoni katika kuboresha Mkakati wa Kitaifa wa Uendelevu wa NGOs nchini ili kuwezesha kuwa na Mkakati bora ambao utazisaidia NGOs kuweza kujiendesha na kutekeleza miradi hata kama kutakosekana wafadhili.
Dkt. Chaula aliongeza kuwa shabaha ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini yanafanya kazi katika mazingira mazuri na kuhakikisha yanachangia katika kuchochea uchumi wa nchi na kuleta ustawi wa jamii .
“Ndio maana Rais Samia akaunda Wizara hii na kuipa nguvu sekta hii ya NGOs na kuweza kuiratibu vizuri zaidi na kuhakikisha inaleta mchango mkubwa kwa Taifa hasa kutoa ajira katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo” alisema Dkt. Chaula
Kwa upande wake Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Vickness Mayao alisema Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni muhimu katika Taifa na yanachangia katika uchumi wa nchi kutokana na miradi mbalimbali ya maendeleo wanayoifanya na kwa mujibu wa taarifa ya Mchango wa NGOs ya mwaka 2021 jumla ya ajira zaidi ya 8,000 zilitolewa na Mashirika hayo katika kipindi cha mwaka mmoja (2020/21).
“Mchango wa NGOs ni mkubwa sana na hata kwa sasa mchango huo umetambulika katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo kwa kutajwa katika mpango huo” alisema Vickness
Naye Mwenyekiti wa kikosi kazi cha kukusanya maoni kuhusu uendelevu wa NGOs, Nensia Mahenge alisema katika ukusanyaji wa maoni ya Mkakati wa Uendelevu wa NGOs imewapa picha kuwa Mashirika yapo katika makundi mbalimbali, ikiwemo yale yanayoanza kufanya kazi yanayotegemea ufadhili, yaliyopo kwa muda kidogo na mengine yaliyofanya kazi kwa muda mrefu, pia yenye uwezo wa kifedha na kujitegemea hivyo maoni kutoka katika Mashirika haya itasaidia kupambanua mbinu za kuweza kujitegemea kwa NGOs.
“Kupitia mikutano hii ya kikanda tumepata maoni ya kujua namna ya kuweka mikakati ya kutatua changamoto zinazozikabili NGOs katika utekelezaji wa miradi yake kwa kuhakikisha inatoa huduma kwa wananchi na ziwe endelevu na zisikwame kwa namna yoyote ile hata pale itakapotokea changamoto za kiuchumi kutoka kwa wafadhili” alisema Nensia
Nao baadhi ya wadau kutoa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutoka Kanda ya Kati walisema Mkakati huo wa Kitaifa wa Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali utakuwa saidizi katika Sekta na kusaidia NGOs kuweza kuwa na mikakati ya kujitegema na kuwa na uendelevu katika kutekeleza majukumu na miradi ya maendeleo.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Mashirka Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) inaratibu zoezi la ukusanyaji wa maoni kuhusu Mkakati wa Kitaifa wa Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutoka kwa wadau wa NGOs kwa mikoa yote ya Tanzania Bara kwa mfumo wa Kikanda.
0 comments:
Post a Comment