Taasisi ya Elimu
Tanzania (TET), inaendesha mafunzo kazini kwa walimu 120 wa masomo ya ufundi
katika shule za sekondari za serikali na zisizo za Serikali Tanzania Bara na
Zanzibar.
Mafunzo hayo yanafanyika
Mkoani Tanga katika shule ya ufundi Tanga (Tanga technical school) kuanzia
tarehe 20/04/2022 na kutarajiwa kumalizika tarehe 25/04/2022.
Akifungua mafunzo hayo
ya siku sita, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bwana
Ali Khamis amesema, mafunzo hayo yanalenga kuboresha utaalamu wa walimu na
kuwezesha ujifunzaji wa masomo ya michepuo (Ufundi, Biashara, Kilimo na Maarifa
ya nyumbani).
"Napenda
niwakumbushe kupitia kwenu taifa linatarajia kupata wahitimu waliobobea na
wanaoweza kujiajiri au kuajiriwa katika fani mbalimbali ikiwemo ufundi mitambo,
umeme, vifaa vya mawasiliano na ujenzi".Amesema
Ameeleza pia kupitia
mafunzo hayo Serikali inatarajia wanafunzi wakiandaliwa vizuri wataweza
kujiajiri na kutengeneza ajira kwa watu wengine.
Amesema malengo hayo
yakifikiwa, taifa litaweza kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia kwa
kuwa litakuwa na vijana wenye uwezo wa kutumia maarifa ya ufundi katika
kufikiri, kubuni na kuunda vifaa na nyenzo za kurahisisha utekelezaji wa
shughuli za maendeleo.
Ameeleza pia mafunzo hayo yamedhamiria katika kukuza stadi za karne ya 21 ambazo ni mawasiliano, ushirikiano, ubunifu na fikra tunduizi.
Pamoja na mambo mengine,
alisema serikali inaendelea kufanya jitihada kubwa za kutoa mafunzo mbalimbali
kwa walimu ili kuboresha taaluma na utaalamu wao katika masomo mbalimbali
yakiwemo masomo ya ufundi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dkt. Aneth Komba amesema Serikali inatarajia kupitia mafunzo hayo walimu wataimarishwa katika ufundishaji wa masomo ya ufundi kwa kuzingatia ufundishaji na ujifunzaji unaozingatia umahiri.
Ameeleza sababu kubwa ya kuanza na kundi hili la walimu wa michepuo ni kuwa Mihtasari ya masomo hayo iliboreshwa kati ya mwaka 2018 na 2019.
"Kwa kawaida
tunapoboresha Mitaala au Mihtasari, huwa ni muhimu sana kuwapitisha walimu
kwenye maboresho yanayofanyika ili kuwawezesha kutekeleza mtaala kwa
mafanikio" amesema Dkt.Komba.
Aidha amesema ili
mafunzo hayo waweze kuwafikia walimu wote, TET imelenga kushusha mafunzo hayo
katika ngazi za chini/karibu na walimu kwa kuweka mazingira ya wawezeshaji wa
mafunzo endelevu kwa walimu kazini katika ngazi ya shule, klasta na vituo vya
mafunzo ya walimu (TRCs)
Naye Mkurugenzi
Msaidizi, Elimu ya Sekondari, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI) Bi.Hadija Mcheka ameishukuru TET kwa kuendelea kutoa mafunzo
kazini kwa walimu na amewataka washiriki kuyatumia mafunzo hayo watakayopata
kwa ufasaha.
"Tunachopata
tukakitumie ipasavyo tusiende kukaa nayo tu bali tukawape uzoefu wenzetu
tuliowaacha shuleni kufanya kazi kwa ushirikiano na kuyasambaza kwa
wanafunzi." Amesema.
Mwisho ameeleza kuwa Serikali inatarajia kuona ufaulu katika shule unaongezeka kupitia mafunzo hayo.
0 comments:
Post a Comment