Na Mathias Canal, Dodoma
Serikali ipo katika mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo (2014) na uboreshaji wa Mitaala ya Elimu ili iweze kuwajengea wanafunzi stadi na ujuzi mbalimbali ikiwemo ufundi utakaowawezesha wahitimu kuhimili ushindani katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Mara baada ya mitaala tajwa kukamilika ikiwa ni pamoja na manunuzi ya vifaa na mashine mbalimbali za ufundi, Elimu ya Ufundi itatolewa katika Shule za Msingi na Sekondari. Aidha, utaratibu wa kufanya mitihani ya Elimu ya Ufundi na kupata vyeti utaandaliwa kwa kushirikiana na mamlaka husika kama vile Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET).
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo leo tarehe 27 Aprili 2022
bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Hai Mhe Elinikyo Mafuwe
Saashisha aliyetaka kufahamu serikali ina mpango gani kufufua Shule za Msingi za Ufundi zilizopo
Wilaya humo pamoja na kuweka utaratibu kwa Wanafunzi wa Shule hizo kufanya mitihani
na kupata Vyeti.
Waziri
Mkenda amesema kuwa pamoja na mapitio ya Sera na Mitaala, Serikali inaendelea kufanya maboresho
makubwa katika Chuo cha Ualimu Kleruu pamoja na Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya
Ufundi Stadi cha Morogoro (MVTCC) kwa kufanya ukarabati wa miundombinu ikiwemo
ujenzi wa mabweni ya Wanafunzi kwa lengo la kuongeza fursa ya mafunzo kwa Walimu
wa masomo ya Ufundi.
Ameongeza
kuwa Chuo Kikuu cha Sayansi na
Teknolojia Mbeya kimeanza maandalizi ya utoaji wa mafunzo hayo katika ngazi ya
Stashahada katika Elimu ya Ufundi (Diploma
in Technical Education) na Postgraduate
Diploma in Technical Education. “Kwa sasa Mitaala ya Masomo hayo inafanyiwa
kazi na Tume ya Vyuo Vikuu ili kuidhinishwa na kuanza kutumika katika Chuo
hicho” Amekaririwa Prof Mkenda
MWISHO
0 comments:
Post a Comment