METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, April 25, 2022

MAWAZIRI WANENA NA WADAU SEKTA YA USAFIRISHAJI NCHINI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa kikao cha majadiliano kati ya Serikali na Wadau sekta ya Usafirishaji kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano jengo la NSSF, Benjamin Mkapa Tower Jijini Dar es Salaam,

 

Sehemu ya washiriki wakifuatilia hoja zilizokuwa zikiwasilishwa wakati wa kikao cha majadiliano kati ya Serikali na Wadau sekta ya Usafirishaji kilichofanyika Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa akieleza jambo wakati wa kikao hicho.

Sehemu ya Viongozi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na Wawakilishi wa Jeshi la Polisi – Usalama Barabarani wakifuatilia hoja zilizokuwa zikiwasilishwa wakati wa kikao cha majadiliano kati ya Serikali na Wadau sekta ya Usafirishaji. Kushoto ni Kamishna wa Kazi Bi. Suzan Mkangwa.

Mwenyekiti wa Chama cha Umoja wa Madereva Nchini (TADWU), Bw. Shurbert Mbakizao akieleza jambo wakati wa kikao hicho.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa (kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Said Mkumba, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Mhe. Fatma Nyangasa (kulia) wakifuatilia hoja mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa wakati wa kikao cha majadiliano kati ya Serikali na Wadau sekta ya Usafirishaji

PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU

(KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)

Na: Mwandishi Wetu – Dar es Salaam

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako pamoja na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa wamebainisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya Usafirishaji nchini ili kuimarisha na kukuza sekta hiyo.

Hayo yameelezwa Aprili 24, 2022 wakati wa kikao cha wadau wa Sekta ya Usafirishaji kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano jengo la NSSF, Benjamin Mkapa Tower Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika kikao hicho Waziri Ndalichako alieleza kuwa, Sekta hiyo ya Usafirishaji ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi Taifa, hivyo Serikali imekuwa ikichukua hatua madhubuti na kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali za wafanyakazi katika sekta hiyo.

Katika maelezo yake, Prof. Ndalichako alieleza kuwa Serikali inatambua kuwepo kwa changamaoto za wafanyakazi Madereva nchini, hivyo katika kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizopo kumekuwa na utaratibu wa kukaa vikao vya mashauriano na wadau ambao ni Serikali, Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi madereva na Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji. Utamaduni huo wa kukaa pamoja umesaidia kupeana taarifa muhimu na kutatua changamoto kwa pamoja.

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan inazingatia misingi ya utawala bora na kuzingatia umuhimu wa majadiliano kwa lengo la kuimarisha mahusiano mema sehemu za kazi ili kuongeza ufanisi na tija kwa lengo la kuinua uchumi wa nchi na kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi na mtu mmoja mmoja,” alieleza

Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano na majadiliano katika maeneo ya kazi kuwa ndio njia pekee inayokubalika katika ulimwengu wa kazi kwa kuwa na mtazamo wa pamoja wa kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali kwenye maeneo ya kazi.

“Dhamana niliyopewa na Mheshimiwa Rais katika kusimamia sekta ya kazi nchini, niwasihi tuendelee kushirikiana kwa pamoja katika utatu wetu yaani Serikali, Waajiri na Wafanyakazi katika kutambua umuhimu wa kuhitajiana katika sekta hii kwa kuzingatia umuhimu wake na pia kujali maslahi ya pande zote,” alisema

Aidha, Waziri Ndalichako amemtaka Kamishna wa Kazi kufanya kaguzi katika maeneo ya kazi ambayo wafanyakazi madereva hawajalipwa mishahara yao kwa muda mrefu ili kuhakikisha madai hayo yanafanyika.

Sambamba na hayo, amewataka wamiliki wa vyombo vya usafiri ambao hawajatoa Mikataba ya Ajira kwa madereva kuhakikisha wanatekeleza takwa hilo kwa kuwa ni wajibu wa kisheria.

Pia, alisisitiza elimu kuendelea kutolewa kwa makundi hayo kupitia vyama vya wamiliki na madereva ili kupunguza malalamiko na changamoto zilizopo. Pamoja na hayo Waziri Ndalichako amewataka waajiri katika sekta hiyo kuhakikisha wanaruhusu uwepo wa Vyama vya Wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi ili kuleta tija na ufanisi.

“Vyama vya wafanyakazi vinasaidia sana kuleta tija na ufanisi katika maeneo kazi kwa kuwa wafanyakazi hutumia vyombo hivyo kushauriana namna bora ya kutatua changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi wa pamoja,” alieleza

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa alisema kuwa Sekta ya Uchukuzi ni chachu ya ukuaji wa uchumi wa Taifa, hivyo amewataka wafanyakazi katika sekta hiyo kendelea kushirikiana na serikali ili kuchochea ukuaji wa sekta hiyo ya usafirishaji.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Umoja wa Madereva Nchini (TADWU), Bw. Shurbert Mbakizao alieleza kuwa wamefarijika kama madereva kwa namna ambavyo serikali hii imekuwa sikifu katika kuwashirikisha kwenye majadiliano ambayo yamekuwa na tija kuzipatia ufumbuzi changamoto zao mbalimbali ikiwa ni pamoja na masuala ya wafanyakazi kutopewa mikataba ya ajira, nyongeza ya mishahara, posho za safari na manyanyaso.

“Hakuna mtu anayefurahia kugoma, tunajua tukigoma mtu anayeathirika ni dereva, lengo letu la kusitisha huduma tarehe 25 ilikuwa ni kupatia ufumbuzi changamoto  zetu ili waajiri wasikie kilio chetu sisi madereva, Serikali imeweza kusikiliza malalamiko yet una wameahidi kuyapatia ufumbuzi,” alisema

Mkutano huo wa Wadau wa Sekta ya Usafirishaji umefanyika Jijini Dar es Salaam ukishirikisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako pamoja na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa, Naibu Waziri wa Mambo Ndani ya Nchi, Mhe. Jumanne Sagini, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Chande, Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Said Mkumba, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Mhe. Fatma Nyangasa, Wawakilishi wa Jeshi la Polisi – Usalama Barabarani, Viongozi Vyama vya Wafanyakazi Madereva, Viongozi Vyama vya Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji na Madereva.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com